Habari

Khalwale arai Ruto amfute kazi Murkomen, sababu ‘watu wanauawa kama mbwa’

Na SHABAN MAKOKHA May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHINIKIZO zinaendelea kutanda ili Rais William Ruto amwachishe kazi Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kutokana na kuendelea kuzorota kwa usalama nchini.

Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale, amesema kwa miezi sita ambayo Bw Murkomen amekuwa mamlakani, ameonyesha hawezi kazi yoyote ya kiusalama huku Wakenya wakiendelea kuuawa kinyama.

“Kutoka Kakamega hadi Lamu, Baringo na maeneo mengine nchini, watu wanaendelea kuuawa kama mbwa. Hakuna mtu ambaye anahisi yuko salama ilhali waziri anakesha kwenye vyombo vya habari akitoa taarifa ambazo haziwasaidii Wakenya,” akasema Dkt Khalwale.

“Wizara ya Usalama wa Ndani ni kubwa sana kwa Murkomen. Tunaomba Rais Ruto atusikilize na amfute kazi Murkomen ili Wakenya waendelee kuwa salama,” akaongeza Dkt Khalwale.

Alikuwa akiongea wakati wa mazishi ya Roselida Akinyi, mwalimu kutoka Navakholo, ambaye alivamiwa, akaibiwa kisha kuuawa baada ya kutoa pesa katika benki mjini Mumias mnamo Aprili 17.

Seneta huyo alidai matukio ya ukosefu wa usalama yanaendelea kupanda tangu Bw Murkomen ateuliwa kwenye Wizara ya Usalama wa Ndani.

Bw Murkomen alihamishiwa hadi wizara hiyo kutoka ile ya michezo kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na rais miezi sita iliyopita.

Dkt Khalwale alitaja kupigwa risasi na kuuawa kwa Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, kuuawa kwa maafisa wa polisi, kutekwa nyara kwa machifu Marsabit na pia kupigwa risasi kwa wakazi watano Ang’ata Barkoi wiki jana, kama baadhi ya matukio yanayoonyesha Bw Murkomen hawezi kusimamia wizara hiyo.

Kauli yake inakuja wakati ambapo baadhi ya wabunge kutoka Bonde la Ufa nao wamemshutumu Bw Murkomen kwa ukosefu wa usalama eneo hilo na maeneo mengine nchini.

Mbunge wa Baringo Kaskazinini, Joseph Makilap, alisema Bw Murkomen amelemewa na kazi huku akitumia muda wake mwingi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ilhali ukosefu wa usalama unaendelea kushuhudiwa kote nchini.

Bw Makilap alimtaka Rais Ruto amtimue waziri huyo akisema hana heshima kwa jamii zinazoishi ukanda wa kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Waziri huyo mnamo Ijumaa aliwashutumu wakazi wa Arror kwa kushiriki ujangili ambao umepitwa na wakati. Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa kiusalama katika eneo la Kampi Samaki.

“Umma kwa sasa hauna imani na utendakazi wa Murkomen katika Wizara ya Usalama wa Ndani. Rais Ruto anastahili kuchukua hatua na kumfuta kazi Murkomen kwa sababu ameshindwa kuhakikisha kuna usalama na sasa anatishia jamii,” akasema Bw Makilap.

Bw Murkomen kabla ya kuteuliwa kwenye Wizara ya Michezo, pia alihudumu kama Waziri wa Uchukuzi.

Ujangili na mashambulio yanayotekelezwa mara kwa mara na kundi la Al-Shabaab Pwani na Kaskazini mwa nchi ni kati ya changamoto za kiusalama ambazo zimeendelea kuzonga nchi Bw Murkomen akiwa Waziri wa Usalama wa Ndani.