Jamvi La Siasa

Siasa za urithi wa kiti cha Kasipul zaanza siku nne tu baada ya Ong’ondo Were kuuawa

Na CECIL ODONGO, GEORGE ODIWUOR May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma sasa anataka chama cha ODM kimteue mmoja wa wanawe marehemu Charles Ong’ondo Were kuwania kiti cha ubunge cha Kasipul.

Marehemu Bw Were ambaye aliuawa kwa risasi wiki jana, atazikwa Ijumaa hii nyumbani kwake kijijini Kachien, Homa Bay. Hata kabla ya kufukiwa kwake mchangani, siasa zimeanza kuhusu nani anastahili kumrithi katika eneobunge hilo.

Bw Kaluma anataka ashirikishwe katika kumteua mwaniaji wa ODM katika kiti hicho huku akisema familia ya marehemu inastahili kumtoa mmoja wao apewe tikiti ya ODM.

Wanasiasa Newton Ogada, Okindo Majiwa na Philip Aroka ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Bw Were pia wanasemekana wanamezea mate kiti hicho japo hawajajitokeza hadharani.

“Familia ya Were haifai kuachwa izame kutoka kwa ramani ya kisiasa. Hata hivyo, mazungumzo kuhusu nani atapokezwa cheti cha chama kitaandaliwa baadaye,”  akasema Bw Kaluma.

Kabla ya kuandaliwa kwa kura hiyo, itabidi mchakato wa kuteuliwa kwa makamishina na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ukamilishwe.

Kati ya maeneobunge yanayosubiri kuandaa chaguzi ndogo ni Ugunja, Magarini na Banisa na sasa Kasipul inajiunga nayo. Ugunja ilibaki wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa Waziri wa Kawi kisha uchaguzi wa Harisson Kombe Magarini nao ulifutwa na Mahakama ya Juu.

Mbunge wa Banisa Kullow Hassan aliaga dunia mnamo Machi 2025.

Bw Kaluma alisema lazima atakuwa na ushawishi kuhusu nani atapokezwa tikiti ya ODM.

“Nilihusika kwa kumteua Moses Kajwang’ kwenye uchaguzi mdogo wa seneti wa Homa Bay mnamo 2016 na amefanikiwa kuchapa kazi. Msiandae mazungumzo kuhusu nani anastahili kuwa mbunge hapa bila kunishirikisha,” Bw Kajwang’ akamwaambia mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga.

“Siwezi kufanya uamuzi wa mwisho kwa sababu hilo ni jukumu la Baba (Raila Odinga) na Wanga lakini nataka niwe kwenye mkutano huo,” akaongeza.

Imebainika mmoja wa wanawe Bw Were ametambuliwa kama anayeweza kumrithi babake. Iwapo atapokezwa tikiti na ashinde, basi atajiunga na viongozi ambao walipata nafasi za uongozi baada ya jamaa zao kufariki na chaguzi ndogo kuandaliwa

Bw Kajwang’ alipata useneta baada ya nduguye Gerald Otieno Kajwang’ kufariki 2015 naye Mutula Kilonzo Jnr (sasa Gavana wa Makueni) alichukua useneta wa Makueni 2014 baada ya mauti ya babake Mutula Kilonzo.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi alishinda uchaguzi mdogo wa Sabatia baada ya babake kufariki 1989.  Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa naye alishinda ubunge wa Saboti kwenye uchaguzi mkuu wa 2007.

Nduguye alikuwa mbunge wa eneo hilo hadi alipofariki 2003 lakini kwenye uchaguzi mdogo uliofuatia Davis Nakitare alichukua usukani kabla ya kubwagwa na Bw Wamalwa 2007.