Habari Mseto

Ushindi kwa Kenya ikipata idhini ya kuandaa Kongamano la Viazi Duniani

Na WAIKWA MAINA May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA itakuwa mwenyeji wa Kongamano la 13 la Viazi Duniani hatua ambayo inaonekana kama ushindi mkubwa kwa nchi.

Hii ni baada ya Baraza la Kitaifa la Viazi nchini (NPCK) kuomba hafla hiyo iandaliwe Nairobi.

Awali hafla hiyo ilipangwa kufanyika Juni mwaka huu nchini Gdansk, Poland ila sasa itafanyika Oktoba, mwakani na inatarajiwa kuvutia watu zaidi ya 1,000.

“Bodi ya Wakurugenzi ya WPC imekagua ombi rasmi linaloongozwa na Baraza la Kitaifa la Viazi (NPCK) la Kenya kutaka ombi lao la awali liangaziwe upya kwa ajili ya Kongamano lijalo,” alisema Peter Zander.

Rais wa WPC alisema, “Kuandaa Kongamano la Viazi Ulimwenguni kutaleta mambo mengi muhimu ya kuzingatiwa. Kongamano la Viazi Ulimwenguni linalenga kuchangia kukomesha umaskini uliokithiri na kuboresha utoshelevu wa chakula kote ulimwenguni. Kwa kuandaa hafla hii nchini Kenya, tutaangazia umuhimu wa viazi kama zao muhimu la chakula na uwezo wao wa kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi, haswa kwa vijana na wanawake katika sekta hiyo,” asema Rais wa WPC.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NPCK Wachira Kaguongo alisema Kenya iko tayari kwa hafla hiyo.

“Tunafuraha na tunathamini hatua ya WPC ya kukubali ombi letu. Wadau wa Kenya wako tayari kwa hafla hiyo. Tukio hili litawezesha Kenya kuunda ushirikiano utakapwanufaisha wakulima wetu.”