Polisi wachunguza simu tatanishi iliyopigiwa msaidizi wa Ong’ondo Were kabla ya mauaji
SAA nane na dakika arobaini mnamo Aprili 30, simu ilipigiwa msaidizi wa Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were.
Msaidizi huyo, aliyekuwa katika majengo ya Bunge wakati huo, alizungumza na mpigaji simu kwa muda wa dakika moja na sekunde kumi.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa mpigaji huyo kuzungumza na mlinzi wa mbunge huyo.
Siku mbili zilizotangulia, mlinzi huyo alipokea simu kutoka kwa nambari hiyo hiyo.
Lakini simu ya alasiri Aprili 30 imevutia umakini wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa sababu Bw Were alipigwa risasi na kuuawa saa chache baadaye.
Na rekodi binafsi za usajili wa nambari ya simu hiyo zimezua utata zaidi.
Bw Were alipigwa risasi na kuuawa na mtu aliyekuwa kwenye pikipiki gari lake liliposimama katika taa za trafiki katika barabara ya Ngong saa moja na nusu jioni, dakika chache baada ya kutoka Bungeni.
Sasa, wapelelezi kutoka Idara ya Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi ya DCI wanaochunguza mauaji ya Were wamezamia sana simu hii ya kushangaza.
Wachunguzi wanaamini kwamba simu hii, iliyopigwa saa tano tu kabla ya mbunge kupigwa risasi, inaweza kusaidia kufichua siri ya mauaji hayo.
Vyanzo vilivyo karibu na uchunguzi viliambia Taifa Leo kwamba nambari hiyo ilisajiliwa siku tatu tu kabla ya mbunge kuuawa.
Ilimpigia tu msaidizi huyo wa mbunge.
Chanzo hicho kilisema uchunguzi zaidi wa laini hiyo ulibaini kuwa ilisajiliwa kwa jina la mwanamke kutoka Nyanza ambaye wapelelezi wamebaini tayari alikuwa amekufa wakati kitambulisho chake kilitumiwa kusajili laini hiyo.
“Tunataka kujua ni nani huyu mpigaji wa simu na alitaka nini,” alisema mpelelezi mmoja anayefahamu suala hilo. Wachunguzi wanataka kujua walichozungumzia.
Jumatano, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, alipokuwa akijibu maswali ya wanahabari huko Meru, alifichua kuwa baadhi ya watu wanaohojiwa na DCI ni watu wa karibu na mbunge.
Bw Murkomen hakufichua majina ya watu hao.
“Wanahusisha watu ambao kawaida walipaswa kulinda maslahi ya Mbunge. Serikali imejitolea kuhakikisha kwamba wahusika hao, baadhi ambao tayari wamekamatwa na wengine watakamatwa muda wowote kuanzia sasa, watafikishwa mbele ya sheria,” alisema Bw Murkomen.
Mnamo Jumanne usiku, wapelelezi walivamia nyumba moja katika eneo la Chokaa, Nairobi, na kupata bastola mbili na risasi tisa.
Polisi waliwakamata wanaume wawili waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Katika taarifa ya Jumatano, Mkuu wa DCI Mohammed Amin alisema polisi pia walipata viatu vinavyofanana na vile vilivyovaliwa na mmoja wa washukiwa walionaswa na kamera za CCTV karibu na eneo ambalo mbunge alionekana akiweka pesa katika duka la M-Pesa jijini.
Silaha zilizopatikana zimepelekwa kwa wataalamu katika makao makuu ya DCI ili kuthibitisha kama mojawapo ilitumika katika mauaji ya mbunge.
Wakati wa uchunguzi wa mwili, risasi kadhaa ziliondolewa kutoka mwili wake. Maganda mengine ya risasi yalipatikana katika eneo la mauaji.
Bastola moja ambayo hapo awali ilipatikana na DCI kutoka kwa wahalifu waliokuwa wakihangaisha wakazi wa Ngong na Nairobi haikulingana na maganda ya risasi yaliyopatikana kwenye eneo la tukio.