Habari

Zawadi ya Sh1.2 bilioni yamsubiri atakayefichulia Amerika aliko gaidi Abdullahi Banati

Na ANTHONY KITIMO May 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Amerika imetangaza zawadi ya dola milioni 10 (Sh1.29b) kwa yeyote atakayetoa habari au kusaidia kutiwa mbaroni kwa mshukiwa wa ugaidi, Abdullahi Banati.

Banati (pichani) alisemekana kupanga shambulio la Januari 5, 2020 katika kambi ya jeshi ya Manda Bay, Kaunti ya Lamu.

Kupitia kitengo cha Reward for Justice (RFJ), Idara ya Mashauri ya Kigeni nchini Amerika imemtaja Bw Banati kuwa mwanachama wa kundi la ugaidi la Jaysh Ayman linalohusishwa na Al-Shaabab.

Bw Banati ametajwa kuwa mshukiwa mkuu wa kupanga na kutekeleza mashambulio hayo ambapo Wamarekani watatu waliuawa katika mashambulio hayo, pamoja na magaidi wanne.

“Bw Banati ni mmoja wa washukiwa waliohusika katika kupanga na kutekeleza mashambulio mnamo Januari 5, 2020 katika eneo la Manda Bay Airfield na ni kundi ambalo limehusishwa na mashambulizi mengine nchini Kenya na Somalia.

“RFJ imetangaza zawadi ya dola millioni 10 kwa yeyote atakayesaidia kutiwa mbaroni kwa mshukiwa,” kitengo hicho cha serikali ya Amerika kilitangaza hayo mnamo Jumatano.

Kambi hiyo ya Manda ni kituo cha mafunzo na usaidizi wa kiusalama kinachoshirikisha wanajeshi wa Amerika na Kenya katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Kambi hii ya kijeshi iko karibu na kisiwa cha kitalii cha Lamu, kwenye pwani ya Kenya.

Banati ni mshukiwa wa pili kuwekewa kitita kikubwa kama hicho baada ya Maalim Ayman, mkuu wa kundi la Jaysh Ayman ambaye pia alihusishwa na mashambulizi hayo ya Manda.

Kundi la Jaysh Ayman ni kitengo cha wasomi wanaohusika katika ugaidi na kimekuwepo kwa zaidi ya miaka 10.

Kiliundwa mwaka wa 2013 kwa operesheni za nchini Kenya, hasa katika Msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu na kimeshukiwa kuhusika na mashambulio mbalimbali humu nchini na Somalia.

Kutolewa kwa ombi la kutoa habari kuhusiana na Banati ni baadhi ya juhudi za pamoja kati ya serikali ya Kenya na Amerika za kupambana na ugaidi.

Mshukiwa huyo Banati amekuwa akisakwa na idara ya ujasusi nchini kwa kuhusika na mashambulio kadhaa ikiwemo lile la Dusit D2 jijini Nairobi katika mwaka wa 2019, shambulio la Westgate mwaka wa 2013 na lile la Chuo Kikuu cha Garissa.