Makala

TAHARIRI: Upangaji matokeo unafaa kuzimwa

February 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

BAADA ya ufichuzi kuibuka kuwa baadhi ya wanasoka na hata viongozi wa kandanda humu nchini wamekuwa wakiuza mechi za Harambee Stars, pana haja ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuchukua hatua kali za kulainisha hali.

Ripoti za baadhi ya wanasoka wa Harambee Stars kupanga mechi baada ya kulipwa na timu pinzani ili kupoteza mechi kimakusudi zinachipuka siku chache baada ya habari nyingine kama hizo kutokea kuwa baadhi ya makocha na wachezaji wamekuwa wakiuza mechi ili wanakamari wa mchezo wa pata-potea ya spoti washinde pesa.

Habari hizi zinaatua moyo sana hasa kwa mashabiki ambao wamekuwa wakitamani sana kuona Harambee Stars iking’ara kwenye mechi za kimataifa lakini aghalabu matamanio hayo yamekuwa yakigonga mwamba.

FKF yafaa ifahamu kuwa yakini hizi ni dalili za uovu mkubwa unaoendelea katika mawanda ya kandanda humu nchini; pana uwezekano mkubwa kuwa kiwango cha kuuza mechi miongoni mwa timu za Kenya kiko juu na huenda hiyo ndiyo maana viwango vya soka ya Kenya vimekuwa vikishuka kila kukicha.

FKF chini ya kinara wake Nick Mwendwa yafaa ihakikishe kuwa waliohusika wamechunguzwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kisha iweke mikakati ya kuzuia kutokea kwa uovu huo tena.

Yawezekana uovu huo ndio ambao umekuwa ukifanya klabu za Kenya kukosa kung’aa katika mechi za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ambapo Gor Mahia, AFC Leopards, Ulinzi Stars na kadhalika zimekuwa zikiondolewa katika hatua za mwanzo mwanzo za mashindano hayo. Gor pekee ndiyo, katika siku za hivi majuzi, imeanza kuonyesha kufanya jambo kwenye medani ya kimataifa.

Je, ni kitu gani kinachoweza kuwa kinachangia kuwepo kwa uovu huo? Pana uwezekano kuwa malipo mabaya wanayopewa wachezaji wa klabu na hata wakati mwingine kunyimwa haki yao, ndiyo yanayochangia katika kuwepo kwa tatizo hili.

Hii inamaanisha, ni muhimu kwa FKF kubuni mbinu zitakazohakikisha kuwa wanasoka wanalipwa pesa zao kwa wakati nazo klabu ziboreshe mishahara na marupurupu ya wachezaji.

Hilo lifanyike pia katika fani nyinginezo za michezo kama vile raga, voliboli, magongo na kadhalika ili njama za kupanga matokeo zisikike tena.