Maandamano, purukushani viwanda vya sukari vikipokezwa wamiliki wapya kwa miaka 30
SERIKALI wikendi ilitoa usimamizi wa viwanda vyake vya sukari kwa wawekezaji wa kibinafsi kwa kuvikodisha kwa miaka 30 huku wanasiasa, wafanyakazi na wanajamii wakipinga hatua hiyo.
Kwa mujibu wa serikali ambayo imejitetea vikali, kutoa usimamizi wa viwanda hivyo kwa wawekezaji ndiyo mbinu ya pekee ambayo inaweza kutumika kuvifufua.
Waziri wa Kilimo, Mutahi Kagwe, alisema kuwa kuharakisha mchakato wa kuvifufua viwanda hivyo ili kuepuka hasara, usimamizi wao ulitolewa kwa wawekezaji kwa miaka 30 kwenye hafla mbalimbali iliyoandaliwa mnamo Jumamosi Mei 10.
“Tafadhali jipangeni kuwasilisha ripoti na stakabadhi kuhusiana na kukodishwa kwa viwanda hivi katika makao makuu yao. Unatarajiwa kujihusisha na shughuli hiyo kama mtu binafsi,” akasema Bw Kagwe katika barua kwa usimamizi wa viwanda hivyo.
Hata hivyo, kumekuwa na pingamizi kutoka kwa baadhi ya viwanda huku wafanyakazi wa kile cha Nzoia wakipinga kiwanda chao kuwa chini ya usimamizi wa Jaswant Rai.
Wabunge Majimbo Kalasinga (Kabuchai) na Jack Wamboka (Bumula) wameshutumu familia ya Rai kwa usimamizi duni wa viwanda vingine ndiposa wakapinga Nzoia kuwekwa chini ya familia hiyo.
“Ni familia hii ndiyo inahusika na masaibu ya kiwanda cha Mumias na hakuna chochote kizuri ambacho wanaweza kukionyesha tangu wachukue usimamizi wa Kiwanda cha Karatasi cha Webuye mnamo 2020,” akasema Bw Kalasinga.
Katika kile kinachoonekana kama maasi, wakuu wa kiwanda cha Kibos waliwasili kuchukua usukani Chemelil wakiwa wameandamana na maafisa wa polisi kukabili fujo zozote ambazo zingeshuhudiwa.
Wafanyakazi hapo awali walikanusha Chemelil kusimamiwa na kiwanda cha Kibos, wakihofia kazi zao zitakatika.
“Tunadhibitiwa sana na kufuli za milango zimebadilishwa. Hatujui kile kitatokea kwa sababu tunahisi kama wafungwa,” akasema mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kwa hofu ya kuadhibiwa.
Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o, alisema kampuni zilizokodishiwa Chemelil na Muhoroni hazina uzoefu wa kusimamia viwanda vya sukari.
“Tunapinga kabisa mpango wa kukodishwa kwa viwanda hivi kwa kuwa unapuuguza changamoto zao na nia ya umma katika kuimarika kwao. Mpango huo utazikosesha familia mbalimbali mapato,” akasema.
Katika kiwanda cha Sony, kulikuwa na taharuki pale usimamizi ulipotwaliwa na kiwanda cha Busia. Wafanyakazi walizungumza kwa sauti ya chini na ilikuwa dhahiri hawakuwa wakitaka usimamizi mpya.
Hali iligeuka tete pale Mkurugenzi Msimamizi, Martine Dima, alipomfuta kazi Mkuu wa Kilimo, Boniface Omondi, kwa kuchochea wafanyakazi.
“Umekuwa ukitatiza mchakato wa kupisha usimamizi mpya kwa kuwachochea wafanyakazi, washikadau, wanakandarasi. Umekuwa ukiwachochea wazue ghasia na wapinge mwekezaji anayeingia,” akasema Bw Dima katika barua yake.