Mudavadi aitisha pesa zaidi kutetea kortini Wakenya walio jela mataifa ya kigeni
MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi amewaomba wabunge watenge pesa zaidi kwa Wizara ya Kigeni ili serikali iweze kukodi huduma za mawakili kwa Wakenya wanaozuiliwa katika mataifa ya ng’ambo.
Hayo yanajiri huku Bw Mudavadi akitoa onyo kali kwa kampuni bandia za kuwasaidia Wakenya kupata ajira ng’ambo zinazowapunja na kupotosha raia hao, hasa vijana.
Alisema kuwa wamiliki wa kampuni hizo watanaswa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu Wakenya wanaozuiliwa katika magereza ya ng’ambo, Bw Mudavadi aliwaambia wabunge kuwa idadi yao ni zaidi ya 1,000.
Wamezuiliwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ulanguzi wa dawa za kulevya.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni alisema kuwa idadi kubwa ya Wakenya hao wanakosa huduma za mawakili wa kuwatetea, kutokana na uhaba wa mgao wa bajeti.
Bw Mudavadi alisema Bunge la Kitaifa halijatengea wizara hiyo fedha za kutosha ili iweze kuchukua hatua ya kukodisha mawakili wa kuwatetea Wakenya walioko magerezani katika nchi mbalimbali.
Licha ya hayo, serikali imekuwa ikiwekewa presha iwatafutie Wakenya hao huduma za mawakili.
“Tunafaa kukumbuka kuwa japo wajibu wetu ni kuwalinda Wakenya, Bunge halijatupa pesa za kutosha kugharamia huduma za kisheria za kuwasaidia Wakenya kokote waliko,” Bw Mudavadi akaeleza.
“Wakati huu, kuna zaidi ya Wakenya 1,000 wanaozuiliwa katika magereza mbalimbali ya mataifa ya kigeni,” akaongeza.
Bw Mudavadi alisema ingawa Serikali imejitolea kulinda haki za raia wake walioko ng’ambo, siyo rahisi kufanya hivyo kwa kesi zote zinazowakumba.
“Tunaweza kuingilia kati nyakati fulani. Lakini Wakenya hao pia wanafaa kuchukua tahadhari na kukoma kujiingiza katika shughuli zinazoweza kuwaweka taabani,” Waziri huyo akaeleza.
“Tunapasa kuwakumbusha Wakenya kuwa anapoabiri ndege na kuwasili katika nchi ya kigeni, utahitajika kuzingatia sheria za nchi hizo sio zile za Kenya,” Bw Mudavadi akaongeza.