KINAYA: Yachekesha Uganda kulalamika kwamba Wakenya walivuka boda na kupiga kura kwao
SISI si watoto! Watu watazoea kutuacha tujiamulie mambo fulani kama Wakenya. Ikiwa mambo yanagusa maisha yetu moja kwa moja, kuna tatizo gani tukijituma kuyashughulikia ili yaende tutakavyo?
Juzi nimewaona Waganda wakilialia kama watoto eti tumevuka mpaka na kuingia kwao kupiga kura. Sasa hicho ni kitu cha kusababisha mtu atete na kututukana mtandaoni kweli?
Ikiwa Waganda wenyewe hawana hamasa ya kupiga kura, kuna tatizo gani tukiwaonyesha jinsi ambavyo kura hupigwa?
Ilikuwa siku ya uchaguzi wa mashinani wa chama cha Yoweri Kaguta Museveni mwenyewe kiitwacho National Resistance Movement (NRM) na nakwambia Wakenya wanaoishi mpakani na nchi hiyo walituwakilisha vizuri.
Walirauka kama kawaida yao, yaani jinsi wanavyofanya kila siku pombe na bidhaa nyingine zikiwa ghali nchini Kenya, wakaingia Uganda kwa shughuli hiyo muhimu ya kupiga kura.
Walikuwa wengi hivi kwamba uchaguzi huo ulisitishwa ili ‘wageni hawa kwanza warejee kwao’. Sina hakika walirejea wote, lakini kisa hicho kitaingia kwenye kumbukumbu za historia, inakiliwe kwamba tulinia kuwafanyia hisani majirani.
Idadi ya Wakenya waliojitokeza ilikuwa kubwa hivi kwamba wangejichagulia viongozi ambao wangejitakia wenyewe kwa ajili ya maslahi ya pombe, sigara chakula, mafuta na kadhalika.
Walevi wetu wamekuwa wakituwakilisha vizuri huko tangu enzi za ‘Sheria za Mututho’ zilizowazuia kunywa pombe wakati wowote waliotaka.
Walijua Bw John Mututho, aliyekuwa mpananaji dhidi ya vileo, hakuwa na mamlaka yoyote Uganda, na hangewakamata kwa kubeba pombe kwa tumbo.
Hivyo basi? Walivuka mpaka, wakabugia vitu vyao na kurejea Kenya huku wakiimba nyimbo tamu na kukanyaga hatua moja hapa na nyingine kule kana kwamba wakiogopa kukanyaga mstari wa siafu ili wasing’atwe sehemu nyeti!
Usije hapa na kiherehere chako kujaribu kutufundisha sheria, eti ni makosa kupiga kura katika nchi ya jirani na hekaya nyingine kama hizo.
Unadhani hatujui?
Maslahi ya mtu yanapoingia hatarini, Wakenya tunasema na liwe liwalo, kesi baadaye. Ama unataka kuniambia hungetaka fursa ya kujichagulia watu watakaoamua utakula au utalalia mate?
Wajanja wa mpakani wana akili tosha za kujua kwamba watahitaji bidhaa muhimu, hivyo waliamua kutolaza damu na kusubiri wachaguliwe watu wabaya na hatari watakaowazuia kuingia Uganda kuzifuata.
Pengine hata waliona Waganda wamekuwa na kiongozi mmoja kwa miongo minne, wakaamua kuwasaidia kumwondoa kimya-kimya kama wasasi wajanja wanaoingia porini bila fujo wasishtue na kutorosha mawindo.
Ikiwa Wakenya, Waganda na Watanzania tunazaliana, na kamwe hatutangazi mazazi yoyote ya mwanaharamu, kubwa ni kunyweana pombe, kuvutiana sigara na kupigiana kura? Watu wana mchezo sana.
Napendekeza mipaka ya mataifa hayo matatu ifutwe kabisa, mtu aishi na kupiga kura anakotaka. Huenda hiyo ndiyo suluhu ya matatizo mengi yanayotukabili, kuu zaidi tawala duni.