‘Kanisa’ la Freemasons linalofahamika kwa usiri mkubwa lanyakwa kwa deni la Sh19 milioni
OPERESHENI ya Kaunti ya Nairobi ya kukusanya Sh50 bilioni kutoka kwa wanaodaiwa ada za ardhi iliingia siku ya pili Jumatano, huku Ukumbi wa Freemasons wa Grand Lodge of East Africa ukiwa miongoni mwa majengo yaliyolengwa.
Operesheni hiyo iliongozwa na Waziri wa Afya wa Kaunti Suzanne Silantoi.
“Tupo hapa kukusanya ada zetu za ardhi kama sehemu ya juhudi pana kuhakikisha kwamba sote tunatii. Hii itahakikisha kwamba kama Kaunti ya Nairobi, tunaweza kutoa huduma,” alisema Bi Silantoi.
Aliandamana na Afisa Mkuu kutoka ofisi ya Gavana Johnson Sakaja, Bi Priscillah Mahinda, na Afisa Mkuu wa Idara ya Nyumba Bi Lydia Mathia pamoja na maafisa wengine.
Kwa mujibu wa Bi Silantoi, kaunti ina takriban ploti 250,000, ambapo ni karibu 50,000 pekee ambazo zimekuwa zikilipiwa ada.
“Tunataka kuwa wa haki kwa wakazi wa Nairobi wote ili kila mtu alipe kwa huduma anazopokea. Si haki kwamba saluni kwenye soko zinalipa ushuru ilhali wamiliki wa majengo hawafanyi hivyo,” aliongeza Bi Silantoi.
Aidha, alisema kuwa kaunti itaanza kukata huduma kama maji na mifumo ya majitaka kwa majengo na nyumba ambazo hazijalipa ada kwa miaka mingi.
“Hatufunga mali ya wanaodaiwa tu, bali pia tutakata huduma kama maji na mifereji pale inapohitajika.”
Wakati wa kuzindua operesheni hiyo Jumanne, Afisa Mkuu wa Mapato Bw Tirus Njoroge alisema kwamba mwaka huu watakuwa wakali, akiongeza kuwa kipindi cha msamaha kilipuuzwa na mamia ya wamiliki wa ardhi.
“Tumeanza shughuli yetu. Tutafunga nyumba katika ploti nambari 209, inayodaiwa Sh4 milioni. Tutabandika kwenye jengo kuwa jengo hili ni mali ya Serikali ya Jiji la Nairobi hadi deni lote lilipwe,” alisema Bw Njoroge.
Uganda House katika Barabara ya Kenyatta na Chester House katika Barabara ya Koinange zilitajwa siku ya kwanza ya operesheni hiyo.
Bw Njoroge alisema kuwa wamiliki wa ardhi waliokaidi malipo wanapaswa kutarajia kutembelewa na maafisa wa kaunti ambao watawataka kulipa, kwa lengo la kukusanya si chini ya Sh10 bilioni katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
“Tutaingia kwenye majengo, tutasajili wapangaji wote kwenye mfumo wetu wa NairobiPay, na tutawafundisha jinsi ya kufanya malipo. Tutatarajia walipe kodi yao kila mwezi kwa Serikali ya Jiji la Nairobi kikamilifu.”
Bi Silantoi aliongeza kuwa operesheni itaendelea Alhamisi katika maeneo yote ya kaunti, na kusema kuwa ataongoza operesheni hiyo katika eneo la Dagoretti.
Kiasi cha pesa ambacho kaunti inalenga kukusanya, Sh10 bilioni, ni sawa na mapato yote ambayo kaunti hupata kwa mwaka kutokana na mapato ya ndani.