Afya na Jamii

Sababu zinazoweza kufanya mwanamke kukosa hedhi ilhali hana ujauzito

Na PAULINE ONGAJI May 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUNA baadhi ya wanawake ambao wanaweza kukosa hedhi hata kufikia miezi mitatu au zaidi ilhali hawajashika mimba.

Iwapo unakumbwa na shida hii, ni vyema kuchunguza sababu zinazokufanya kukosa hedhi kwa muda huu wote licha ya kuwa wewe si mjamzito. Aidha, ni vyema kubaini chanzo.

Kuna sababu kadhaa zinazochangia kuchelewa au kupotea kwa hedhi licha ya kuwa mwanamke hajashika mimba. Kwa wanawake wengi ambao wametimu umri wa kuwa na uwezo wa kupata watoto, wanashauriwa kuangalia sababu zifuatazo:

Kunyonyesha

Ni kawaida kwa akina mama wengi wanaonyonyesha kukosa kuona hedhi kwa miezi kadhaa hasa baada ya kujifungua, hadi mtoto atakapoanza kula chakula kingine mbali na maziwa ya mama. Hii ni kawaida kwani hupatia mwili wa mwanamke muda wa kurejelea hali yake ya kawaida.

Kuongeza au kupunguza uzani ghafla

Kuongeza au kupunguza kiwango kikubwa cha uzani kunaweza pia kusababisha kuchelea au kutoweka kabisa kwa hedhi. Hali hii huathiri shughuli za kawaida za mwili wa mwanamke, ikiwa ni pamoja na kalenda ya siku za kawaida za kupata hedhi. Kufanya mazoezi kwa wingi pia, kunaweza changia shida hii.

Msongo wa akili

Mawazo mengi hasa kwa siku kadha mfululizo, yana uwezo wa kutatiza shughuli za mwili wa mwanamke na hivyo kusababisa hali hii. Lakini, mawazo haya yakipungua, hedhi huonekana muda mfupi baadaye. Kupumzika na kutuliza mawazo pia, kunaweza rejesha hali ya kawaida.

Umri

Ni kawaida kwa msichana anapopata hedhi kwa mara ya kwanza maishani, kukosa kwa miezi kadhaa baadaye, licha ya kuwa hajashika mimba. Hedhi huchukua muda wa angalau miaka mitatu tangu siku ya kwanza kuonekana, kuzoea mwili wa mwanamke. Pia, ni kawaida kwa wanawake ambao tayari wamepitisha umri wa makamo, kukumbwa na shida hii.

Mbinu za upangaji uzazi

Kwa wanawake walio na mazoea ya kumeza tembe za upangaji uzazi kwa wingi, ni kawaida pia kwao kushuhudia mabadiliko haya mwilini. Hii ni kutokana homoni zinazopatikana kwenye tembe hizi, ambazo zina uwezo wa kuathiri shughuli kamili za mwili.

Matumizi ya dawa

Kuna dawa ambazo zina uwezo wa kuathiri kiwango cha homoni mwilini na hivyo kupelekea kutoweka kwa hedhi.

Ugonjwa

Ni kawaia kwa magonjwa kuathiri shughuli za kawaida mwilini, na hivyo kuchangia tatizo hili. Lakini, pindi mgonjwa anapopata nafuu, hedhi hurejea kama kawaida.

Ili kurejesha hali ya kawaida ya kuwa na hedhi, wanawake wanashauriwa kufanya yafuatayo:

· Kuwa na lishe bora kwani, chakula bora kina uwezo wa kusaidia mwili kufanya shughuli zake za kawaida bila matatizo.

· Tumia virutubishi vya vitamini, kufuatana na maelezo kutoka kwa daktari.

· Dawa za kienyeji zilizoidhinishwa kwa minajili ya kusafisha damu mwilini pia zaweza kupunguza shida hii.

Iwapo mbinu hizi hazitafaulu, ni vyema kutafuta ushauri kutoka kwa daktari. Aidha, ni vyema kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini iwapo umeshika mimba au la kabla ya kuchukua hatua hizi.