Rais wa zamani wa Gabon, familia watorokea Angola
ALIYEKUWA Rais wa Gabon Ali Bongo, 66, ambaye aliondolewa mamlakani kwa njia ya mapinduzi 2023, usiku wa kuamkia Ijumaa alisafiri kwa ndege na familia yake kupata hifadhi Angola.
Bongo, mkewe Sylvia Bongo, 62 na mwanawe Noureddin, 33 mapema wiki hii waliondolewa gerezani na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani. Wamekuwa wakizuiwa tangu Agosti 2023 wakishutumiwa kwa kushiriki uhalifu ikiwemo ufujaji wa mali na ulanguzi wa fedha.
Ali Bongo, 66 mwenyewe awali aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani baada ya mapinduzi hayo. Baadaye aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Hata hivyo, wafuasi wake walipinga hayo wakisema amekuwa akizuiliwa wala hajawai kuondoka Libreville. Duru ziliarifu familia ya Bongo Iliondoka usiku wa kuamikia Alhamisi.
Sylvia na Noureddin Bongo walihamishwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mnamo Mei. Walikuwa wakizuiliwa kwenye seli za chini katika ikulu ya rais.
Japo wafuasi wao wamekuwa wakisema walipigwa na kuteswa kwenye kizuizini, Rais Oligui Nguema ambaye aliongoza mapinduzi hayo amekanusha hilo. Waziri wa Mawasiliano wa Gabon Paul-Marie Gondjout hajazungumzia suala hilo.
Nguema aliapishwa kwa muhula wa miaka saba mwezi huu baada ya kushinda uchaguzi kwa asilimia 95.
Mnamo Aprili 30, Baraza la Usalama na Amani katika Umoja wa Afrika (AU) liliresha Gabon kwenye umoja huo. Gabon iliondolewa kwenye AU kutokana na mapinduzi yaliyomwondoa Ali Bongo madarakani.
Kupitia taarifa, AU ilitoa wito kuachiliwa kwa familia ya Ali Bongo na hakikisho kuwa haki zao pamoja na afya yao italindwa. Kabla ya kuondolewa 2023 na rais wa sasa kupitia mapinduzi ya jeshi, AIi Bongo alikuwa ameongoza tangu 2009.
Hii ni baada ya kuchukua mamlaka kutoka babake aliyekuwa ameaga dunia baada ya miaka 40 afisini.