Habari Mseto

Polisi watakiwa kuvumilia mgao mdogo ili aliyewajengea hospitali alipwe Sh833 milioni

Na DAVID MWERE May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WABUNGE sasa wameamua kukata Sh833.60 milioni kwenye pesa zilizotengewa bima ya polisi ili kumlipa mwanakandarasi aliyejenga Hospitali ya Polisi karibu na Mbagathi, Nairobi kwa kima cha Sh1.23 bilioni.

Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Masuala ya Ndani imesema pesa hizo (Sh833.60 milioni) zitatumika kumlipa mwanakandarasi huyo ili hospitali hiyo ianze kutumika.

Hospitali hiyo itakabidhiwa kwa Huduma ya Kitaifa kwa Polisi (NPS) ambayo ilitenga Sh8.7 bilioni kwa bima ya polisi  kuanzia Aprili 1 hadi Machi 31, 2026.

Kampuni za APA na Joint Venture ndizo zilipewa tenda za bima hiyo ya polisi kwa kima Sh8.7 bilioni.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo Gabriel Tongoyo ambaye ni mbunge wa Narok Magharibi, hospitali hiyo ilikamilishwa miaka miwili iliyopita, ina vitanda 150 na vifaa vyote na lazima ianze kutumika.

Mwanakandarasi alitekeleza ujenzi na kuweka vifaa alikuwa amekataa kuiachilia kwa serikali kutokana na deni la Sh833.60 milioni baada ya serikali kulipa Sh400 milioni pekee.

Bw Tongoyo na mbunge wa  Saku Dido Raso ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati hiyo,  walisema gharama ya matibabu itashuka iwapo polisi wataanza kutibiwa katika hospitali hiyo kuliko kuhudumiwa kwenye hospitali za kibinafsi.

“Tunaona mmetenga Sh12 bilioni kwa bima ya polisi ila hamna chochote kulipa deni la mwanakandarasi wa hospitali iliyokamilishwa na iko tayari kutoa huduma,”  Bw Tongoyo akamwambia Inspekta Jerenali wa Polisi Dougas Kanja na Katibu wa NPS anayehusika na utawala Bernice Lemedeket.

Wawili hao walikuwa wamefika mbele ya kamati hiyo kutetea bajeti yao ya 2025/26.

“Mbona msitumie pesa za bima kumaliza deni la hospitali ambayo imemalizika na polisi hawapati huduma,” akaongeza Bw Tongoyo.

Kilichowashangaza wanachama wa kamati hiyo zaidi ni kauli ya Bi Lemedeket kuwa Sh200 milioni zimetengwa kuwalipa wahudumu kwenye hospitali hiyo ilhali bado haifanyi kazi.