Kimataifa

Tanzania yazima mawasiliano kwa mtandao wa X baada ya akaunti ya Polisi kudukuliwa

Na CHARLES WASONGA May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SAA chache baada ya wahalifu wa mitandaoni kudukua akaunti ya mtandao wa X wa Idara ya Polisi Tanzania, serikali ya nchi hiyo imejibu kwa kuzima matumizi ya mtandao huo wa kijamii.

Shirika la NetBlocks linalofuatilia mawasiliano kwa njia ya intaneti Jumatano Mei 21, 2025 lilisema hatua hiyo ilichukuliwa saa chache baada ya tukio hilo Jumanne.

Data za shirika hilo zilionyesha kuwa huduma za X (zamani twitter) zilikuwa chini katika mashirika ya kutoa huduma za intaneti (ISPs) kote nchini Tanzania kama vile Halotel, Airtel, Liquid Telecom, Habari Node na Vodacom.

“Imebainika kuwa mtandao wa X hauwezi kutumika kupitia mashirika ya kutoa huduma za mawasiliano ya intaneti nchini Uganda. Hayo yanajiri baada ya akaunti ya X ya Idara ya Polisi kudukuliwa na kutumiwa kupitisha habari za kupotosha kwamba Rais amekufa, hali iliyokasirisha serikali,” ikasema NetBlock yenye makao yake jijini London, Uingereza Jumanne saaa tatu za usiku, saa za Afrika Mashariki.

Akaunti ya X ya Idara ya Polisi Tanzania ilidukuliwa Jumanne, Mei 20, 2025 asubuhi na ikaanza kupitisha habari za kupotosha kama viloe kwamba Rais Samia Suluhu amefariki.

Hata hivyo, baada ya muda serikali ilirejesha udhibiti wa akaunti hiyo, ambayo hufuatiliwa na zaidi ya watu 470,000, na kutangaza kuwa inawaandama wahusika katika katika uhalifu huo.

Akaunti ya X ya Idara ya Polisi ya Tanzania ilidukuliwa baada serikali ya nchini hiyo kuelekezewa shutuma kwa kuwazuilia na kuwarejesha makwao wanaharakati na mawakili kadhaa waliowasili nchini humo kuhudhuria kesi ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.

Kesi hiyo ilitajwa Jumatatu Mei 19, 2025 zaidi ya mwezi mmoja tangu kiongozi huyo wa chama cha CHADEMA kukamatwa na kuziuliwa korokoroni mnamo Aprili 9, 2025.

Miongoni mwa waliozimwa kuhudhuria kesi hiyo ni kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua, Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Hussein Khalid, Hanifah Adan, Lynn Ngugi na Gloria Kimani.

Wanaharakati wengine Boniface Mwangi (kutoka Kenya) na Agather Atuhaire (kutoka Uganda) wamekuwa wakizuiliwa jijini Dar es Salama na maafisa wa kijeshi na hatima yao haijulikani.

Hata hivyo, shirika la kimataifa la kutetea haki Amnesty International lilisema serikali ya Tanzania ilikuwa imepanga kuwafurusha wawili hao na kuwarejesha makwao.

Mnamo Jumatano jioni Rais Suluhu alizungumzia suala hilo na kusema kwa serikali yake haitawaruhusi wanaharakati kutoka mataifa ya kigeni “kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania”.

“Wameharibu kwao na hatutawaruhusu kuja hapa kwetu kuharibu mambo. Hilo halitafanyika,” Mama Suluhu akasema alipoongoza hafla ya uzinduzi wa hati ya sera za kigeni za Tanzania.

Rais huyo ambaye ameshutumiwa kwa kurejeshwa Tanzania katika utawala wa kidikteta wa mtangulizi wake John Magufulu, alisisitiza kuwa maafisa wa usalama wa Tanzania, “hawataruhusu watu kutoka nchi zingine kuchochea watu wetu.”