Dimba

Punguzeni kikosi au niondoke Man City, Guardiola afoka

Na REUTERS May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City ametishia kujiuzulu klabuni humo iwapo wasimamizi wake hawatapunguza idadi ya wachezaji, huku akidai kwamba idadi hiyo kubwa inamchanganya wakati anapounda kikosi.

“Sifurahii ninapolazimika kuwaacha wachezaji wengi nje wakati wa kupanga kikosi,” Guadiola alisema hayo baada ya kutowapa nafasi kikosi mastaa wake kadhaa wakiwemo Abdukodir Khusanov, Savinho, James McAtee, Claudio Echeverri na Rico Lewis mnamo Jumanne usiku, Man City walipocheza na Bournemout na kuibuka washindi kwa magoli 3-1 dhidi ya Bournemouth ugani Etihad.

Mabao hayo yalifungwa na Omar Marmoush dakika ya 14, Bernard Silva (38), na Nico Gonzalez (89). Mateo Kovacic alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 67.

Daniel Jebbison aliifungia Bournemouth katika dakika ya mwisho muda wa ziada (90+6).

“Tayari nimewaambia sitaki idadi kubwa ya wachezaji, kwa sababu sitaki kuacha nje wachezaji watano hadi sita kwenye baridi. Sitaki kabisa. Nitaondoka iwapo hawatachukua hatua ya kupunguza idadi hiyo.

“Inakuwa vigumu kuwaambia wachezaji kwenye mazoezi kwamba hawawezi kucheza. Katika mipango yangu ya kukibadilisha kikosi, pengine nitahitaji tu walinzi kwa sababu safu hiyo ndiyo iliyokuwa na ulegevu,” aliongeza mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 54 ambaye mkataba wake na klabu hiyo unamalizika 2027.

“Kama kocha siwezi kunoa wachezaji 26 halafu wanne, watano au sita wanabakia nyumbani kwa sababu hawawezi kucheza. Sitakubali hilo. Niliwaambia wakuu wa klabu kuhusu hilo, na sitaki kurudia.”

Mwaka huu ulipoanza City walitumia zaidi ya Sh34.5 bilioni kununua wachezaji wapya, wakiwemo Khusanov, Marmoush, Gonzalez na Vitor Reis, huku wengine wakiwasili kwa mkopo, lakini hawajawa wakipata nafasi ya kucheza.

Kevin de Bruyne ndiye mchezaji wa pekee aliyethibitisha kuondoka baada ya msimu huu kumalizika wikendi hii, lakini hali ya kiungo mwenzake Jack Grealish haijulikani baada ya kuendelea kukosa nafasi kikosini.

“Heri wajipange kama Chelsea ambao wana idadi ya wachezaji 31, huku wengine 21 wakiwa nje kwa mikataba ya mikopo.”

Ugani Selhurst Park usiku huo, Crystal Palace ambao majuzi walitwaa ubingwa wa FA Cup kwa kuchapa City 1-0, waliendeleza ubabe wao kwa kuichapa Wolves 4-2, wafungaji wao wakiwa Eddie Nketiah (2), Ben Chilwel na Eberech Eze, wakati yale ya Wolves yakimiminwa wavuni na Emmanuel Agbadou na Jorgen Strand Larsen.

Katika mechi ya Man City, mashabiki wa klabu hiyo walimkaribisha kiungo mahiri, Rodri baada ya kukaa nje kwa miezi minane kutokana na jeraha la gotini (ACL) alilopata wakicheza na Arsenal Septemba mwaka uliopita.

Nyota huyo alikaribishwa kwa nderemo na vifijo alipoingia kubadilishana na Erling Haaland dakika ya 83.

Mara tu staa huyo mwenye umri wa miaka 28 alipoumia, Man City walianza kuyumbayumba kwenye kampeni yao ya kutetea ubingwa wa EPL huku wakilazimika kukabidhi taji hilo kwa Liverpool ambao walitwaa ubingwa zikibakia mechi nne.

Rodri alituzwa taji la Mchezaji Bora la Ballon d’Or akiwa kwenye mikongojo mwaka jana. Alizoa taji hilo baada ya kuisaidia Uhispania kutwaa taji la Euro 2024. Pia aliisaidia City kutwaa taji la Klabu Bora Duniani.

Baada ya ushindi wa Jumanne, City wanakamata nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 68 huku wakilenga kushiriki michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Timu tano bora za Uingereza zitafuzu huku ushindani mkali ukishuhudiwa kati ya timu ya tatu hadi ya saba.