Kenya sasa yaingilia kati, yataka Tanzania kumwachilia huru Mwangi
SERIKALI ya Kenya imevunja kimya kuhusu kutoweka kwa Mwanaharakati Boniface Mwangi, akiwa nchini Tanzania.
Katibu wa Wizara ya Masuala ya Nje, Dkt Abraham Korir Sing’Oei, amelalamikia kutoweka kwa Bw Mwangi na akaiomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtoa au kumwachilia.
“Wizara inabaini kuwa licha ya maombi kadhaa, maafisa wa serikali ya Kenya wamezuiwa kupata taarifa na pia kumfikia Bw Mwangi. Wizara pia ina wasiwasi kuhusu hali yake ya afya, ustawi wake kwa ujumla na ukosefu wa taarifa kuhusu kuzuiliwa kwake,” alisema Katibu huyo katika taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.
Katibu huyo aliomba serikali ya Tanzania kuheshimu na kufuata Mkataba wa Vienna kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia (1963), unaosema kuwa maafisa wa kibalozi wanapaswa kuwa huru kuwasiliana na raia wa nchi zao na pia kuwa na haki ya kuwatembelea.
Aliongeza kuwa mkataba huo pia unasema kuwa maafisa hao wanapaswa kuruhusiwa kumtembelea raia wa nchi yao akiwa gerezani, korokoroni au kizuizini, kuzungumza naye, kuwasiliana naye na kupanga uwakilishi wa kisheria kwa niaba yake.
“Kutokana na hayo, Wizara ya Masuala ya Nje na Wakenya wanaoishi nje ya nchi inaiomba kwa heshima Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuruhusu mara moja maafisa wa ubalozi wa Kenya kumpata Bw Mwangi au kumwachilia huru kwa mujibu wa wajibu wa kisheria kimataifa na taratibu za kidiplomasia,” alisema Katibu huyo.
Vilevile, Katibu huyo alisisitiza kuwa serikali ya Kenya imejizatiti kudumisha uhusiano mzuri wa pande mbili kati ya mataifa hayo mawili.
Bw Mwangi alitoweka Jumanne, siku moja baada ya kudai kuwa maafisa wa polisi walikuwa wamepiga kambi nje ya chumba chek katika hoteli moja.
Alikuwa amesafiri kwenda Tanzania pamoja na wanaharakati wengine kuonyesha umoja wao na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye alifikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.
Licha ya kuruhusiwa kuingia nchini humo, Bw Mwangi hakuweza kufika mahakamani wakati Bw Lissu alipofikishwa mbele ya hakimu.
Wanaharakati wa Kenya wameungana na serikali kulaani hatua ya serikali ya Tanzania kumkamata.
Hivi majuzi, Rais wa Tanzania alisema hataruhusu watu kutoka mataifa mengine kuleta vurugu nchini mwake.
“Tumeanza kuona mwenendo ambapo baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani wanajaribu kuingilia mambo yetu. Kama wamekomeshwa kwao, basi wasije kuvuruga amani yetu hapa,” alisema Mama Suluhu.
Awali, Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Nje Musalia Mudavadi aliunga mkono kauli ya Rais Suluhu.
“Sitalalamika kuhusu hilo kwa sababu nafikiri kuna ukweli. Tukubali baadhi ya mambo. Kiwango cha lugha chafu, matusi tunayoona Kenya, ingawa tuna uhuru wa kujieleza, wakati mwingine kinavuka mipaka. Anachosema ni kuwa watu wakati mwingine wamevuka mipaka katika matamshi yao nchini Kenya, na hilo ni kweli,tunachopaswa kuzungumzia ni, tunawezaje kuelewa kilichotokea huko, ukweli ni kuwa mitazamo yetu na matamshi yetu, kwa sababu ya uhuru wa kujieleza, imekosa uadilifu,” alisema Waziri huyo katika mahojiano ya televisheni siku ya Jumanne.