Masumbwi yafanyika Charter Hall
MABONDIA hodari kutoka mataifa mbali mbali ikiwemo nchi jirani za Tanzania na Uganda ni miongoni walioidhinishwa kushiriki kwenye mashindano ya masumbwi ya kulipwa Ijumaa (Mei 23,2025) katika ukumbi wa Charter Hall jijini Nairobi.
Mashindano hayo ya siku moja chini ya udhamini wa 12 Sports Rounds Promoter ya Stephen Sembuya vile vile yanayotarajiwa kuvutia mashabiki wengi huku muundo wa teknolojia za kisasa ukitumika ili kuhakikisha kuwa mashabiki wanafurahia mtazamo wa kipekee kupitia njia ya kidijitali.
Sembuya ambaye ni raia wa Uganda anayeishi Amerika amehamisha shughuli zake za kuandaa mapigano Nairobi baada ya kuwekewa masharti magumu nchini mwake.
Kwa ushirikiano wa Tume ya Ngumi za Kulipwa Nchini (KPBC) inayoongozwa na Reuben Ndolo, mashabiki watanunua tiketi zao kwa Sh500 (kukaa sehemu ya kawaid), Sh1,500 (VIP) na Sh3,000 (VVIP).
Akizungmza na waandishi wa habari za michezo baada ya shughuli za mabondia kupimwa afya jana, Ndolo alisema mbali na kusaidia mabondia kuimarisha rekodi zao, vile vile wanalenga kukuza masumbwi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ndolo alisema mashindano kama haya yatatangaza utalii wa Kenya kwa vile yanajumuisha mabondia kutoka mataifa ya kigeni, akiwemo Adam Belaida wa Algeria anayeishi Sweden.
Alisema wageni waliofika nchini vile vile watapata fursa ya kuzuri nchini kujionea hifadhi za kitaifa, mbali na kuchangia katika ukuzaji wa mchezo huu kwa jumla.
Akizungmza kwa njia ya simu akiwa Amerika, Sembuya alisema amejitolea kusaidia mabondia kupalilia vipaji vyoa ili watambulike kimataifa, mbali na kujenga rekodi zao.
Alipeana mfano wa bondia Henry Kasujaa wa Uganda ambaye alianza masumbwi ya kulipwa mnamo 2022 na kuimarika haraka haraka hadi kufikia kiwango cha Mkenya, Rayton Okwiri aliyeanza kuzipiga 2017.
Mabondia wengine waliopitia mikononi mwake na kupiga hatua ya haraka ni Suleiman Segawa na David Ssemuju.
Katika mapigano ya leo, Kasujaa amepangiwa kuchapana na Charles Misango wa Malawi kwenye pigano la raundi 10.
Ndolo alitoa mwito kwa mashabiki wajiandae mapema kupata tiketi zao ili waipuke msongamano wa dakika za mwisho.