Habari

Amerika yataka uchunguzi ufanywe kuhusu madai ya mateso ya wanaharakati

Na ELVIS ONDIEKI May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUKAMATWA na madai ya kuteswa kwa wanaharakati kutoka Kenya na Uganda nchini Tanzania kumevutia hisia za Amerika, ambayo imetaka uchunguzi wa haraka ufanyike mara moja.

Mnamo Ijumaa, Idara ya Masuala ya Afrika ya Amerika, inayofanya kazi chini ya Wizara ya Masuala ya Kigeni, ilichapisha ujumbe mkali kwenye mtandao wa X kulalamikia jinsi Boniface Mwangi wa Kenya na Agather Atuhaire kutoka Uganda walivyotendewa.

“Amerika inasikitishwa sana na ripoti za ukatili dhidi ya wanaharakati hawa wawili wa Afrika Mashariki wakiwa Tanzania,” ilisema.

Iliongeza kuwa Bi Atuhaire alitambuliwa mwaka jana na Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika kama mshindi wa tuzo ya Wanawake Jasiri Kimataifa (International Women of Courage).

“Tunaomba uchunguzi wa haraka na wa kina kufanyika kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu. Tunahimiza nchi zote za ukanda kuwajibisha wahusika wote wa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo mateso,” ulisema ujumbe huo.

Taarifa hiyo ilichapishwa tena na ubalozi wa Amerika jijini Nairobi Jumamosi asubuhi.

Amnesty International pia iliunga mkono wito wa uchunguzi.

“Serikali ya Tanzania lazima ichunguze kukamatwa kiholela, kuteswa, kuzuiliwa bila mawasiliano, na kutimuliwa kwa watetezi wa haki za binadamu,” ilisema taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa Amnesty International eneo la Afrika Mashariki na Kusini, Bw Tigere Chagutah, alisema: “Kwa siku nne, watetezi hawa wa haki za binadamu waliteswa kikatili. Kisa hiki kinaonyesha hatari wanazokumbana nazo watetezi wa haki nchini Tanzania na lazima kuwepo na uwajibikaji na haki. Amnesty International inataka uchunguzi wa kina uanze mara moja.”

Shirika hilo la haki za binadamu pia lilikosoa matamshi ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu baada ya wanaharakati hao kukamatwa huku wengine wakifukuzwa mapema wiki hiyo.

“Amnesty International inatiwa wasiwasi na matamshi ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kukamatwa kwa wanaharakati hao, alipotisha kuwachukulia hatua watetezi wa haki za binadamu wanaoingia Tanzania, akiwaita ‘maajenti wa kigeni’. Kauli kama hizi zinapatia maafisa wa serikali sababu zisizo halali za kuweka vikwazo vinavyokiuka wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu,” ilisema. “Amnesty International imeripoti ongezeko la unyanyasaji wa wapinzani wanaodumisha amani katika miaka ya hivi karibuni huku nchi ikielekea kwenye uchaguzi wa rais na wabunge unaotarajiwa Oktoba 2025.”

Bi Atuhaire alitupwa eneo la Mutukula, karibu na mpaka wa Uganda na Tanzania baada ya kutoweka kwa siku kadhaa.

Kwa upande mwingine, Bw Mwangi alitupwa Ukunda, eneo la Pwani karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania. Kabla ya kupatikana kwake, Kenya ilikuwa imetoa taarifa ikisema kuwa Tanzania haikuwa ikishirikiana katika kufichua alikokuwa Bw Mwangi.

Wanaharakati hao wawili walikuwa wameenda Tanzania kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani wa Tanzania Tundu Lissu iliyofanyika Jumatatu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Kupitia chapisho la Facebook Ijumaa, Bw Mwangi alieleza mateso waliyopitia.

“Mara ya mwisho kuwa naye (Bi Atuhaire) katika eneo moja ilikuwa Jumanne asubuhi. Tulikuwa tumeteswa, tuliambiwa tuvue nguo zote na kuagizwa tuoge,” alisema.

“Hatukuweza kutembea, tuliambiwa tutambae kuosha damu. Tulifungwa pingu na kufungwa macho, kwa hivyo sikuweza hata kumuona, lakini nilimsikia akiguna kwa maumivu walipokuwa wakitupigia kelele. Tulipojaribu kuzungumza usiku huo wa mateso tulipigwa mateke na kutukanwa. Tuliondolewa eneo la mateso kwa magari tofauti,” aliongeza Bw Mwangi.

Aliongeza pia: “Waliotutesa walikuwa wakitekeleza maagizo ya afisa wa usalama wa taifa aliyefika katika ofisi za Uhamiaji na kutufuatilia hadi Kituo Kikuu cha Polisi na kuamuru tupelekwe hadi eneo la siri ili ‘tupatiwe huduma ya Kitanzania’. Mtu huyo alinipiga mbele ya mawakili watatu kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika.”