Wito serikali iingilie kati madereva wanaozuiliwa Sudan Kusini waachiliwe
Chama cha Madereva na Makondakta wa Masafa Marefu (LoDCA) sasa kinasema kuwa serikali ya Kenya imekataa kuingilia kati suala hilo licha ya kuongezeka kwa maombi ya usaidizi.
Mwenyekiti wa LoDCA Roman Waema alisema licha ya uingiliaji kati wa chama hicho, kumekuwa na mfadhaiko kutokana na kusitasita kwa serikali ya Kenya kuingilia kati kwa niaba yao.
Bw Waema alisema licha ya baadhi kulipa faini, bado wako katika magereza nchini Sudan Kusini huku wengine wakizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka rasmi katika taifa hilo.
“Kinachotukatisha tamaa zaidi ni licha ya Bw Mohammed Ahmed (dereva) kulipa Sh29 milioni baada ya lori lake kuhusika katika ajali iliyosababisha vifo vya watu 11 bado hajaachiliwa,” akasema Bw Waema.
Aliongeza, ‘Tumemwandikia barua kadhaa Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi na kuzuru Juba kushinikiza kuachiliwa kwa wenzetu akiwemo Bw Ahmed, ambaye amelipa fidia kwa waliohusika katika ajali hiyo.’
Bw Waema pia alimtaja Bw Abdi Mohammed, ambaye pia yuko jela licha ya kulipa faini zake zote za trafiki.
“Tulikutana na Naibu Rais wa Sudan Kusini Benjamin Bol Mel, ambaye aliahidi kuokoa Wakenya, ambao wako gerezani lakini inaonekana ni machache sana yanayofanywa huku wenzetu wakiteseka gerezani,” alisema mwenyekiti wa chama hicho.
Kulingana na madereva hao wa lori, madereva wa Kenya na wenzao wengine kutoka eneo hilo wanaishia kwenye jela za Sudan Kusini kutokana na makosa madogo madogo, ambayo yanatokana na usanifu mbaya wa barabara katika taifa hilo la kigeni.
Chama hicho kilidai madereva wa kigeni wanaohusika mara nyingi wanakabiliwa na michakato ya muda mrefu ya mahakama isiyo na msingi wazi wa kisheria ambapo kupata uwakilishi wa kisheria ni vigumu, na maamuzi mara nyingi yanapendelea maslahi ya ndani.
LoDCA inahoji kuwa dosari hizi za kimfumo zinaunda mazingira ya uhasama, ambapo matokeo ya kisheria yanategemea uamuzi wa maafisa badala ya sheria iliyowekwa.
”Wakati matukio ya trafiki yanapoongezeka na kuwa taratibu za kisheria, madereva wa kigeni wanakabiliwa na vita kali. Uwakilishi wa kisheria ni vigumu kupata, kesi mahakamani zinaenda polepole, na maamuzi mara nyingi yanapendelea maslahi ya ndani. Baadhi ya madereva wamejikuta wakifungwa kwa miezi kadhaa bila kufunguliwa mashtaka rasmi, kwa sababu tu hawakuweza kutimiza matakwa ya ‘fidia’ yaliyotolewa na wahusika au viongozi husika,’ kilisema chama hicho.
Wakati huo huo, madereva hao wa malori wamelaumu kukosekana kwa kanuni bora chini ya Umoja wa Forodha wa EAC, wakibainisha kuwa ingawa mamlaka ya umoja huo yalioanisha sera za usafiri wa barabarani, mamlaka za Sudan Kusini mara nyingi huweka sheria holela ambazo zinakinzana na makubaliano ya kikanda.