Trump aita Putin punguani kwa kushambulia Ukraine
NEW JERSY, Amerika
RAIS wa Amerika Donald Trump amesema amekerwa na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin baada ya taifa hilo kufanya mashambulio mabaya zaidi nchini Ukraine.
Huku akimkaripia vikali Putin, Trump alisema: Nini kimemfanyikia? Anawaua watu wengi zaidi?”
Baadaye Rais huyo wa Amerika alimwita Putin “Mwendawazimu wa kupindukia”.
Awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema unyamavu wa Amerika baada ya mashambulio ya hivi karibuni yanayotekelezwa unampa moyo Putin, akipendekeza presha kali iwekewe Urusi ikiwemo vikwazo.
Watu 12 waliuawa na wengine wengi wakajeruhi Jumapili usiku baada ya Urusi kushambulia Ukraine kwa droni 367 na makombora- idadi kubwa zaidi usiku mmoja tangu Urusi ilipovamia Ukraine mnamo 2022.
Jana asubuhi, ving’ora vilivyoashiria ujio wa droni na makombora vilisikika tena katika sehemu mbali mbali za Ukraine.
Watu watatu, akiwemo mtoto, walijeruhiwa katika mji wa Kharkiv, ulioko eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, Meya Ihor Terekhov akasema.
Katika eneo la Zaporizhzhia, lililoko kusini mwa Ukraine, watu wawili walijeruhiwa,” akasema afisa mkuu wa utawala wa Ivan Fedorov.
Nchini Urusi, Meya wa Moscow Sergei Sobyanini alisema droni za Ukraine zilizokuwa zikielekea jijini humo, ziliharibiwa na wanajeshi wa kikosi cha angani.
Hakuna majeruhi walioripotiwa.
Akiongea na wanahabari New Jersey Jumapili jioni, Trump alimrejelea Putin hivi: “Nimemjua kwa muda mrefu na kushirikiana naye mara kadhaa, lakini anakosea kwa kutuma roketi katika miji ya Ukraine na kuua watu. Daima nitachukia kitendo hicho.”
Alipoulizwa ikiwa anapanga kuiwekea Urusi vikwazo zaidi, Trump alijibu: “Bila shaka.”
Awali, Rais huyo wa Amerika amekuwa akitishia kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi, lakini kufikia sasa hajatekeleza tishio hilo.
Trump alimtaka Rais Putin kukomesha uchu wake wa kutaka kudhibiti maeneo yote ya Ukraine akionya kuwa hatua hiyo “itasababisha kuangamia kwa Urusi.”
Ukosoaji
Lakini Rais huyo wa Amerika pia alimrushia maneno makali Rais Zelensky, akisema haisaidii nchi yake kwa njia yoyote ile kwa “kuongea zaidi”.
“Maneno yote anayotamka huleta shida. Sipendi hilo na sharti akome,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu Zelensky.
Licha ya kwamba wandani wa Ukraine katika bara Uropa wanajiandaa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi, Amerika imesema itaendelea kusimamia mazungumzo ya amani, au ijiondoe ikiwa juhudi zake hazitaonekana kuzaa matunda.
Wiki jana, Trump na Putin walifanya mazungumzo kwa saa mbili, kwa njia ya simu, kujadili mkataba wa amani uliopendekezwa na Amerika kukomesha mapigano hayo.
Rais wa Amerika alisema mazungumzo hayo yaliendelea vizuri zaidi akiongeza kuwa Urusi na Ukraine zinatarajiwa kuanzisha mazungumzo kwa lengo la “kukomesha vita”.
Ukraine imekubali kwamba mapigano yasitishwe kwa kipindi cha siku 30.
Lakini Rais Putin alisema tu kwamba Urusi itashirikiana na Ukraine kuandaa “memoranda” kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungunzo, hatua ambayo Ukraine na wandani wake barani Uropa waliitaja kama inayolenga kuchelewesha mazungumzo hayo.