Habari

Wezi wavunja kanisa, wafurahia sakramenti, divai na kuiba mali

Na George Munene May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAJAMBAZI walivunja kanisa jingine katika kaunti ya Kirinyaga na kuiba mali ya thamani ya Sh120,000 usiku wa Jumapili Mei 25, 2025.

Majambazi hao pia walikula sakramenti na kunywa divai ya kanisa katika uvamizi wa kijasiri uliotekelezwa katika Kanisa la Kianglikana la Mtakatifu Mathayo Mutithi, jambo lililowaacha waumini katika mshtuko mkubwa.

Baada ya karamu hiyo ya wizi, majambazi walitoroka na mali waliyoiba, wakiacha dirisha la kanisa limeharibiwa.

Kwa mujibu wa viongozi wa kanisa, wanachama wa kwaya walipowasili katika nyumba hiyo takatifu asubuhi ya Jumatatu kwa ibada walikuta vifaa kama kinanda, ngoma na mali nyingine havipo.

Majambazi waliingia ndani ya kanisa kwa kuvunja dirisha, kutekeleza uhalifu wao na kutoroka bila kugunduliwa.

“Majambazi waliingia ndani ya kanisa kupitia dirisha na kuiba mali; tukio hili la uhalifu limetuacha tukiwa na mshangao mkubwa,” alisema makamu mwenyekiti wa kanisa, Bw Kithaka Muriuki.

Muumini mmoja, Bi Ruth Wangui, alisema wizi huo unaonyesha wazi kuwa majambazi hawana heshima kwa maeneo takatifu.

“Ni dhambi kuiba mali iliyowekwa kwa kumtumikia Mungu, wezi hawa watajiletea laana kutoka kwa Mungu,” alisema Bi Wangui.

Wimbi jipya la uhalifu linalolenga makanisa limeongezeka katika eneo hilo, hali ambayo imesababisha wasiwasi kwa viongozi wa kiroho na waumini wao.

Wezi wanavunja makanisa na kuiba vifaa vilivyokusudiwa kwa ibada.

Kanisa la Redeemed Gospel Church katika Eneo Bunge la Gichugu pia lilivunjwa na mali kuibwa.

Majambazi walivamia kanisa hilo usiku wa Jumamosi na kuiba vifaa vya maelfu ya pesa. Pia waling’oa mlango wa chuma wa thamani ya Sh30,000 kutoka jengo la kanisa na kutoroka na mali hiyo.

Waumini na viongozi wa kanisa walipofika kanisani siku ya Jumapili walipatwa na mshangao kuona mlango na vifaa vya mahubiri havikuwepo.

“Ni huzuni kwamba majambazi walivunja kanisa na kuiba mali; makanisa sasa yanalengwa na wahalifu,” alisema Mchungaji Mercy Munyi.

“Ilikuwa ibada ya kuchosha kwa sababu vifaa vyetu vya mahubiri viliibwa na majambazi,” alisema Mchungaji Munyi.

Mnamo Januari 19, majambazi walivunja Kanisa Anglikana la Kitharaini na kuiba maikrofoni, vipaza sauti na na vifaa vingine vya thamani ya Sh300,000.

Viongozi wa kanisa walisema wezi hao pia waliharibu kanisa kwa kiwango kikubwa, wakisababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba hiyo ya ibada.

“Yaliyotokea katika kanisa letu yamewaacha wengi na mshangao. Inaonekana majambazi hawa hawamwogopi Mungu,” alisema mmoja wa viongozi wa kanisa, Bw Daniel Muriithi.

Na mnamo Septemba 5 mwaka jana, wezi walivamia Kanisa la Anglikana la Ichang’i na kuiba mali ya thamani ya maelfu ya pesa.

Viongozi wa kanisa walisema uvamizi huo ni sawa na kukufuru maeneo takatifu na wanaiaka polisi wa eneo hilo kudhibiti wahalifu hao.

“Tumeripoti tukio hili kwa polisi na tumerekodi taarifa; sasa tunasubiri kuona kama hatua zitachukuliwa,” alisema Mchungaji Munyi.

Viongozi wa kanisa walisisitiza kuwa ni laana kutia najisi makanisa ambayo waumini hukusanyika kumuabudu Mungu na kutoa sadaka takatifu.

“Isipokuwa wavamizi hawa watubu, hawataepuka adhabu ya Mungu,” alisema kiongozi mwingine.

Viongozi hao wa kanisa walisema majambazi hao wanalenga kuvuruga kazi ya Mungu lakini wakatahadharisha kuwa siku zao zinahesabika.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kirinyaga Mashariki, Bw Johnson Wachira, alisema uchunguzi kuhusu uvamizi huo umeanza.

Tayari washukiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na uvamizi wa Kanisa la Kitharaini.

“Tumewakamata washukiwa wawili na mlango wa chuma pia umepatikana. Washukiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema.