Habari

Wanahabari watishiwa maisha kwa kufichua kamari haramu ya kidini

Na DANIEL OGETTA May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAHABARI wawili wa kampuni ya Nation Media Group (NMG), wamepokea vitisho kufuatia makala ya upekuzi yaliyofichua jinsi majukwaa ya kidini yanavyotapeli watu kwa kuendesha kamari haramu iliyojificha katika vipindi vya imani.

Waandishi hao wameomba polisi waanzishe uchunguzi “kwa lengo la kutathmini iwapo mashtaka ya jinai yanaweza kufunguliwa dhidi ya wanaohusika na vitisho hivyo.”

Bw Ibrahim Karanja na Bw Fred Muitiriri, ambao wote ni wanahabari wa runinga, walikuwa sehemu ya timu ya upekuzi iliyoonekana kwenye makala ya runinga yaliyopeperushwa kupitia NTV kwa kichwa Madhabahu ya Kamari (Kiswahili) na Sacred Swindle (Kiingereza) mnamo Mei 25, 2025. Toleo la makala hayo liliandikwa na mwandishi Steve Otieno na kuchapishwa siku iliyofuata.

Bw Karanja na Bw Muitiriri wamepokea vitisho kwa nyakati tofauti, vinavyohusishwa moja kwa moja na nafasi yao katika uchunguzi huo.

“Tayari wamepokea taarifa zinazoweza kuaminiwa kuhusu vitisho au tabia fulani katika mazingira yao zinazowatia hofu kuwa huenda watu fulani wanapanga kuwatendea madhara,” inasema barua ya malalamishi iliyowasilishwa kwa Kamanda wa Polisi wa Nairobi, Bw George Seda.

Kulingana na Mkuu wa Kitengo cha Kisheria cha NMG, Bw Sekou Owino, “hali hiyo imechochewa zaidi na ukweli kuwa kila mmoja wa wanahabari hao amepokea simu nyingi kwa nambari zao binafsi, lakini wanaozipiga wanabaki kimya wakipokea simu hizo.”

Barua hiyo inaongeza kuwa wanahabari hao sasa wana hofu kuwa watu walioanikwa katika makala hayo huenda wananuia kuwatisha au kuwatendea madhara.

“Hii ni kutoa taarifa rasmi kwa ofisi yako kuhusu hofu waliyo nayo wanahabari hao kuhusu vitisho dhidi ya usalama wao wa kibinafsi na maisha yao, na kuomba ofisi yako iingilie kati kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha vitisho hivyo ili kuzuia uwezekano wao kudhuriwa,” alisema Bw Owino.

Aidha, alifafanua kuwa “wanahabari hao wako tayari kushirikiana katika uchunguzi kwa kurekodi taarifa au kutoa maelezo na nyenzo nyingine zitakazosaidia ofisi yako katika kufanya uchunguzi huo.”

Baada ya makala hayo kupeperushwa, Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) siku ya Jumatatu ilitambua uzito wa madai yaliyofichuliwa, ambayo yaliwataja baadhi ya watangazaji na hasa kampuni ya Yahweh’s Media Services Limited pamoja na vituo tanzu vyake kwa kupeperusha matangazo ya kamari haramu chini ya kivuli cha vipindi vya kidini.

Kama hatua ya kurekebisha hali hiyo, CA ilitangaza kutumia Kifungu cha 83A cha Sheria ya Mawasiliano ya Kenya ya mwaka 1998 kuadhibu kila mtangazaji aliyekiuka kwa kumtoza faini ya Sh500,000 na kuwapa muda wa saa 12 kusitisha mara moja matangazo yote yasiyo halali.