• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Sahau urais wenye mamlaka makuu, Kuria aambia Ruto

Sahau urais wenye mamlaka makuu, Kuria aambia Ruto

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Moses Kuria amemtaka Naibu Rais William Ruto kusahau urais wenye mamlaka ilivyo kwa sasa akisema sharti katiba ifanyiwe mabadiliko ili kubuniwe wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili.

Alisema bali na naibu rais, rais atahitaji usaidizi kutoka kwa waziri mkuu na manaibu wawili ili kuendesha serikali itakayotekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Nashukuru Naibu Rais kwa kuunga mkono marekebisho ya katiba. Lakini napinga mfumo wa sasa unaowaweka watu wawili kileleni mwa serikali huku wale wengine wakitumia nguvu zao kuwapiga vita. Tunataka mamlaka makuu kugawanywa kati ya watu watano, ambao naamini watatoka makabila mbalimbali,” Bw Kuria akasema kwenye ujumbe wa Facebook.

“Hii kitu hakuna mtu ataikula peke yake tena. Hiyo imepitwa na wakati,” akasisitiza akiongeza kuwa anatumai kuwa hivi karibuni Dkt Ruto atakumbatia wazo maarufu kama “Super 5 ticket.”

Akihutubu Ijumaa katika ukumbi wa Chatham House, London, Uingereza, Dkt Ruto aliunga mkono marekebisho ya katiba lakini akapinga kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili.

“Siungi mkono wanaopendekeza kuundwa kwa nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka kwa sababu hiyo haitasaidia kusuluhisha shida tunayokabiliana nayo sasa ambapo anayeibuka wa pili katika kura za urais “huachwa nje bila kupata nafasi yoyote ya uongozi unaotambulika kikatiba” akasema.

Dkt Ruto akaongeza, “Chaguzi za urais nchini hushuhudia ushindani mkali ambapo aghalabu anayechukua nambari mbili hupata zaidi ya kura milioni tano. Si vyema kwa mtu kama huyo kuachwa nje lakini hafai kupewa wadhifa wa waziri mkuu.”

Naibu Rais pia alisema endapo wadhifa huo utaundwa bado hautasuluhisha shida ya kutokuwepo kwa uongozi jumuishi kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwamba cheo hicho kitatwaliwa na chama kilichoshinda urais.

Dkt Ruto anapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

ambao utashikiliwa na mgombeaji urais atakachoibuka nambari mbili . Na pamoja na mgombeaji mwenza wake watakuwa wabunge.

“Na ninapendekeza kuwa Kiongozi Rasmi wa Upinzani pia awe ndiye Kiongozi wa Upinzani Bungeni huku Naibu Rais akiwa Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Mfumo kama huu pia ukumbatiwa katika ngazi ya serikali za kaunti ambapo manaibu gavana watatekeleza majukumu hayo katika mabunge ya kaunti,” akasema.

Lakini japo Dkt Ruto anapinga kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kutokana na gharama kubwa ya kufadhili zoezi hilo, utekelezaji wa mapendekezo yake yatabadili muundo wa uongozi wa nchi. Na kulingana na kipengee ch 255 cha katiba mabadiliko kama hayo sharti yaidhinishwe na wananchi kupitia kura ya maamuzi.

Na akitetea wazo la kubuniwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili Bw Kuria alisema hatua hiyo italeta utulivu nchini “bila kupunguza mamlaka ya Rais au kuanzisha mfumo wa bunge.”

“Kimsingi, ni demokrasia yenye upekee wa Kenya,” akasisitiza.

Bw Kuria huyo ambaye tayari amewasilisha mapendekezo yake kwa Kamati ya Maridhiano (BBI) alisema kubuniwa kwa nafasi tatu zaidi kileleni mwa uongozi, haina gharama kama vile kuwepo wa maseneta 16 maalum, wabunge 12 maalum, wabunge wawakilishi wa kaunti 47 na zaidi ya madiwani 1,000 maalum, “ambayo tunapaswa kufutilia mbali.”

You can share this post!

Ukapera hauathiri kazi yangu, asema Mbunge

Sonko ajitolea kwa hali na mali kumuunga Kalonzo 2022

adminleo