Habari MsetoSiasa

Sonko ajitolea kwa hali na mali kumuunga Kalonzo 2022

February 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BERNARDINE MUTANU

GAVANA wa Nairobi Gideon Mbuvi ametangaza kumuunga mkono kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka kuwania urais 2022.

Akiongea wakati wa mkutano mkubwa wa viongozi na wakazi kutoka Ukambani, Bw Mbuvi alisema atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa Bw Musyoka ametwaa uongozi na kuahidi kufadhili kampeni yake ya ‘kukutana’ na wananchi.

Bw Mbuvi ni mwanachama wa Jubilee lakini katika hotuba yake wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Eneo Bunge la Matungulu, Komarock, alionekana kuegemea uongozi wa Bw Musyoka 2022.

“Mimi namuelewa Rais zaidi kushinda mtu mwingine yeyote hapa, afadhali waseme mimi ni mtu wa mkono wa Rais. Kwa yale mambo ya salamu, mimi naelewa mheshimiwa Kalonzo ndiye atakuwa mstari wa mbele. Na sisi tutakuwa nyuma yake,” alisema.

Aliendelea, “Mimi kwa sasa, sina haja ya kusimama kiti cha urais, haja yangu ni kuona wewe Kalonzo ambaye umetutangulia, tukusaidie mpaka wakati utastaafu au uwe mzee.”

Bw Mbuvi alisema anaelewa muafaka na kwamba Bw Musyoka yumo ndani ya huo mkataba licha ya dhana kuwa alitengwa na viongozi hao wawili.

Aliahidi kutumia pesa kufadhili mikutano mikubwa inayoongozwa na Bw Musyoka na pia kutoa kikundi chake cha Sonko Rescue Team kumfanyia kampeni.

“Juzi, Uhuru na Raila walifanya handshake, nataka niwaambie siri ya ‘handshake’, Mheshimiwa Kalonzo yuko ndani,” alisema na kuwakosoa magavana wa Ukambani ambao kwa muda wamekuwa wakimkosoa kiongozi huyo wa Wiper.

Aliwataka kumheshimu Bw Musyoka na kuungana na viongozi wengine katika kuunganisha jamii ya Wakamba.

“Umoja ni muhimu sana kwa kila jamii. Wakati Raila Odinga alienda Nyanza akiwa na Rais, niliona magavana wote wa Nyanza hapo, wabunge na pia wawakilishi wa wadi. Mimi kama gavana wa Nairobi, nitafanya kila kitu nihakikishe watu wa jamii yetu wanaungana pamoja na tayari nimeanza,” alisema.

“Ninawaomba wale magavana wenzangu watatu, lazima tumheshimu Kalonzo Musyoka. Ninawaheshimu lakini nitawatafuta ili tuunganishe jamii yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa ikiwa wakazi wa Nairobi, ambao wametoka makabila mbali mbali wanaweza kumpigia kura kwa pamoja,itakuwaje jamii ya Wakamba mashinani haiwezi kumuunga mkono Bw Musyoka kwa pamoja?

“Na yule ambaye anaita Kalonzo mtu wa mkono, aachane na hayo matusi, sisi tunajua matusi kuliko mtu yeyote hii Kenya. Wakati Raila alienda na Uhuru kufanya maendeleo Nyanza, alikuwa mtu wa mkono wa Uhuru? Hivyo watu wawe na heshima,” aliongeza.

Pia aliitaka jamii ya Wakamba kugeuza mbinu kwa lengo la kutambulika katika uongozi nchini.