• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Wakazi wang’ang’ania ngano na madereva baada ya ajali ya trela

Wakazi wang’ang’ania ngano na madereva baada ya ajali ya trela

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa Free Area, Nakuru waling’ang’ania unga wa ngano baada ya mtu mmoja kupoteza maisha yake na mwingine kujeruhiwa katika ajali iliyotokea katika barabara ya Nairobi kuelekea Nakuru, Jumatatu.

Trela ya kubeba mizigo, KAB 206A, ilipoteza mwelekeo baada ya kumgonga mpita njia aliyefariki papo hapo.

Hatimaye lori hilo lilipatana ana kwa ana na gari dogo la shirika la kibinafsi linalomilikiwa na International Organisation Migration (IOM)

Kulingana na walioshuhudia mkasa huo, dereva wa lori alijaribu kumkwepa mpita njia lakini badala yake akamgonga.

Magunia ya ngano yaliyotapakaa kando ya njia shughuli za kuokoa majeruhi zikiendelea. Madereva wa baadhi ya magari ya uchukuzi wa umma wanatuhumiwa kupora magunia ya ngano. Picha/Richard Maosi

Dereva wa lori alitoweka muda mfupi baadaye akihofia hasira za wakazi.

Magunia ya ngano yalitapakaa njiani, huku vijana kutoka mtaa wa Freearea wakijishindia mali ya bure.

Madereva wa magari ya uchukuzi wa umma wasiokuwa na huruma, kutoka mitaa ya Lanet na Pipeline, hawakubaki nyuma kwani walianza kupakia magunia kadhaa ndani ya magari yao.

Polisi waliofika katika eneo la tukio walikuwa na wakati mgumu kutawanya watu waliotatiza shughuli za uokozi na kusababisha msongamano mkubwa wa magari, yaliyolazimika kuchukua mkondo tofauti.

Baadhi ya vijana walionyakua magunia ya ngano walikabiliwa na polisi.

Barabara ya Nakuru Nairobi imekuwa ikishuhudia visa vya ajali za kila mara, wakazi wakinyoshea serikali kidole cha lawama kwa kuwapuuza.

Polisi wakishika doria katika eneo la ajali barabara ya Nakuru kuelekea Nairobi siku ya Jumatatu. Picha/ Richard Maosi

Kwa mujibu wa Nathan Mwangi, mkazi wa Freearea, sehemu hiyo haina alama za barabara kuwaelekeza madereva na wapita njia.

“Hatuna sehemu maalum ya kuvukia njia,hasa wanaotaabika zaidi ni watoto wa shule za msingi wanaohitaji kusindikizwa,”Nathan alisema.

Naibu kamishna wa polisi, kaunti ya Nakuru Daniel Kitavi alisema visa vya ajali vimepungua,siku za hivi karibuni.

“Ajali nyingi hutokea kwenye matuta ya barabara kwa sababu hazina alama za kuelekeza madereva,” alisema.

You can share this post!

JAMVI: Ishara huenda Uhuru asiondoke mamlakani 2022

Uhuru awatuza waliobwagwa uchaguzini

adminleo