Wanaopinga uongozi wa askofu AIPCA waombwa kujiengua
Na LAWRENCE ONGARO
KANISA la African Independent Pentecostal Church Of Africa, (AIPCA) lina kiongozi na hakuna pengo la uongozi, ndilo tamko la Askofu Mkuu wa kanisa hilo Bw Julis Njoroge Gitau.
Amewataja viongozi wengine wa kanisa hilo ambao wanajaribu kumng’oa uongozini kama wenye tamaa ambao hawatafanikiwa.
“Kwa muda wa miezi mitano hivi tuliketi na kikundi hicho na tukakubaliana kuwa ni vyema kuwatumikia waumini wetu na mwongozo moja badala ya malumbano, lakini wengine wetu hawakutilia hayo maanani,” alisema Askofu mkuu Bw Gitau.
Alisema kikundi cha waasi kilifanya juhudi hata kuandikia Rais Uhuru Kenyatta barua na pia afisi ya msajili wa afisi ya Mkuu wa Sheria.
“Lakini kulingana na msajili wa maswala ya sheria anatambua afisi yetu kama halali ambayo imesajiliwa rasmi kuendesha maswala ya kiroho kwa waumini wetu.
Huku akihutubia waandishi wa habari askofu mkuu Bw Gitau alisema wapinzani wake ambao pia wanatambulika kama maaskofu wana haki kuendesha mambo yao kivyao bila kuvuruga kanisa linaloendeshwa kihalali la AIPCA.
Alisema sasa ni wakati wake wa kutumikia waumini wake kwa kuwalisha chakula cha kiroho na kwa hivyo hangetaka kuona watu wachache wenye tamaa ya uongozi wakimhangaisha.
Maafisa halali wanaostahili kuendesha kanisa hilo kirasmi ni katibu mkuu ni Stanely Mburu Mwangi, naye mwenyekiti wake ni Paul Watoro Gichu.
Katibu mkuu Bw Mwangi alisema ya kwamba cha muhimu ni kwamba hawamshurutishi mtu yeyote kuendelea kuwa mshiriki wa AIPCA, iwapo mtu anajisikia kuondoka ana nafasi kufanya hivyo wakati wowote.
“Hata hivyo sisi kama maafisa wakuu wa kanisa hili tunatoa mwito ya kwamba iwapo unafikiria kugura kanisa hili na kuanzisha chako pahali pengine ni lazima utaacha mali yote ya kanisa letu ili uwe huru kufanya utakalo kwingine,” alisema Bw Mwangi.
Alisema kanisa linamtambua askofu mkuu Bw Gitau ambaye amechaguliwa kihalali na kwa hivyo ni sharti kila mmoja aheshimu mwelekeo huo badala ya kuchochea waumini.
Wakati wa kikao hicho waumini na maafisa wengi walifika katika kanisa la AIPCA la Thika ili kumtambua Askofu mkuu Gitau kama kiongozi wao rasmi na hawamtambui mwingine.
Naye Mwenyekiti Bw Gichu alisema kuwa kwa muda wa miaka 20 wamekuwa wakifuata katiba ya kanisa ipasavyo na kwa hivyo yeyote asiyetosheka anastahili kuja kwa maafisa waliochaguliwa na kanisa ili wazungumze kama watumishi wa Mungu.
“Ni vyema kukubali wakati mwingine kuongozwa wala sio kutaka kuongoza bila kupewa nafasi na waumini. Kazi ya Mungu ni ya kunyenyekea wala sio ya mabavu,” alisema Bw Gichu.
Alisema sheria ya kanisa inasema ya kwamba Askofu mkuu ni kiongozi wa kanisa ambaye huchaguliwa kila baada ya miaka mitano na kwa hivyo walio na uchu wa uongozi wangojee hadi miaka hizo zikamilike ili kujiwasilisha kwa wahusika.