Kenya mbioni kujenga kituo cha utafiti wa sayari
Na CAROLYNE AGOSA
SERIKALI ya Kenya iko mbioni kujenga kituo cha kwanza kabisa cha kuangalilia sayari angani kama vile mwezi na nyota, katika eneo la Turkana.
Kituo hicho kinachotazamiwa kuwa cha kipekee Afrika kinatazamiwa kukuza elimu na sayansi ya angani kupitia utafiti humu nchini huku kikiwa kivutio cha utalii kwa Wakenya na wageni. Ni taifa la Afrika Kusini pekee barani lenye kituo cha kuangalilia sayari.
Kinatarajiwa kugharimu kati ya Sh149.39 milioni na Sh398.37 milioni huku ujenzi wake kuchukua miaka mitano.
Hata hivyo, mradi huo unakumbwa na changamoto za kifedha huku ufadhili wa sasa ukikatika Machi baada ya awamu ya pili kukamilika.
Ufadhili huo wa pamoja kutoka Kenya na Uingereza umetolewa kupitia Tume ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi (NACOSTI) ya Kenya na Hazina ya Utafiti na Uvumbuzi kuhusu Changamoto za Ulimwenguni (GCRF) ya Uingereza.
“Kenya inakumbwa na uhamaji mkubwa wa wasomi na wataalamu wa sayansi na teknolojia kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kukuza talanta zao kwa manufaa ya taifa,” alisema Prof Paul Baki, Mkuu wa Idara ya Fiziki na Sayansi ya Angani katika Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK).
“Ukosefu huo umesababisha sayansi ya angani kusalia kuwa elimunadharia bila kuletea taifa matunda yake halisi,” alisema.
Dkt Martyn Wells kutoka Kituo cha Teknolojia ya Sayansi ya Sayari Angani nchini Uingereza alisikitika kwamba Kenya iko na rasilimali asili ya kutosha kwa sayansi ya angani kunawiri.
“Kenya inajivunia moja ya anga nzuri sana Afrika ya kuangalilia sayari za angani wakati wa usiku, na bora kuliko hata mataifa mengine ya Ulaya. Lakini rasilimali hii haitumiki.
“Vile vile, hakuna vifaa vya kuwasaidia wasomi wa fizikia na hesabu kukuza utaalamu wao kwa manufaa ya taifa,” alisema Dkt Wells ambaye ndiye anaongoza hazina ya GCRF.
Anga wazi, mawingu machache mno mwaka mzima, na hali ya hewa isiyobadilika sana ni baadhi ya sifa ambazo alisema Kenya inajivunia katika eneo la Kaskazini.
Sifa hizo ndizo zimefanya maeneo mawili yaliyo Turkana kuchaguliwa kama pendekezo la makazi ya kituo hicho kipya, huku ukaguzi zaidi ukitarajiwa kufanywa ili kuteua moja.
Dkt Nadir Hashim alihimiza serikali ya kitaifa kuhusika zaidi katika kituo hicho akisema sayansi ni kichocheo cha umoja wa taifa.
“Kituo hiki kitakuwa na manufaa si haba kwa taifa. Wakenya kutoka kila pembe watajumuika kwa pamoja kutalii kituo hicho na hapo kukuza utangamano,” akasema Dkt Hashim ambaye ni mwenyekiti wa Idara ya Fizikia katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Kituo hicho, aliendelea, pia kitasaidia kukuza zaidi mvuto wa sayansi ya angani hapa nchini na kuwezesha wananchi kushuhudia matukio ya angani vyema zaidi, kama vile kuzuiwa kwa mwanga wa mwezi au jua (eclipse).
Aidha, kitaimarisha kiwango cha elimu ya sayansi kwani wanafunzi watapata pahali pa kushuhudia mambo kwa uhalisi. Tayari mradi huo umejumuisha wanafunzi kadha kutoka shule mbalimbali kama njia ya kukuza ufahamu wao wa sayansi ya angani.
Ujenzi wa kituo hicho utachangia kuimarisha miundo msingi ya eneo hilo, kuletea wakazi ajira na fursa za uwekezaji, kukuza utalii, na mwishowe kuimarisha uchumi wa hapo.
Wataalamu wa sayansi ya sayari walikuwa wakizungumza siku ya mwisho ya kongamano la kimataifa la wataalamu na wadau wa sayansi ya sayari angani lililokamilika Alhamisi mjini Nairobi.
Kongamano hilo lilihitimisha msururu wa mikutano na shughuli za awamu ya pili ya mradi itakayotamatika mwezi ujao ufadhili ukinyauka.
Chimbuko la mradi huo lilianza mwongo mmoja uliopita baada ya Dkt David Buckley, kutoka kituo cha uangalizi cha Afrika Kusini, kutua nchini kufanya utafiti wa maeneo yanayoweza kuwekwa kituo hicho.
Utafiti huo ulifanywa kwa ushirikiano na wanasayansi wenzake kadha na Chuo Kikuu cha Inoorero.
Aidha, katika awamu hii mafunzo maalum ya sayansi ya angani yalitolewa kwa wanasayansi kadha wa humu nchini.
Awamu ya pili ilihusu uteuzi wa maeneo mawili kutoka kwa orodha ya maeneo 13 yaliyo sehemu mbalimbali nchini, yatakayofanyiwa ukaguzi zaidi ili kuchagua moja itakayokuwa makazi ya kituo cha uangalizi sayari angani.
Maeneo hayo mawili yaliyoteuliwa yanapatikana katika eneo pana la Turkana: Ol Donyo Nyiro na Mount Kulal.
Wataalamu watafanya ukaguzi zaidi na uchanganuzi wa kina wa data za setilaiti na mashinani za hali ya hewa katika maeneo hayo ili hatimaye kuteua eneo moja kuwa makazi ya kituo.