Magunia 222 ya bangi yanaswa Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

BANGI yenye thamani ya mamilioni ya hela ilinaswa katika jumba la kifahari eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu.

Kamanda mkuu wa polisi katika eneo hilo Bw Adiel Nyange, alisema polisi wa Kahawa kwa ushirikiano na wakazi wa eneo hilo walivamia jumba hilo na kunasa magunia 222 za uzito wa kilo 1,100 za thamani ya Sh 4.5 milioni.

Alisema wakazi wa eneo hilo walishuku lori fulani majira ya usiku wa Jumatatu, na baadaye waliona magunia kadha yakiondoshwa kwenye Lori hilo na kuingizwa katika nyumba hiyo.

“Ninashukuru ushirikiano mzuri uliofanywa kati ya wananchi na polisi na hiyo ndiyo ilisababisha bangi hiyo kunaswa. Ningetaka ushirikiano huo udumu zaidi,” alisema Bw Nyange.

Alijulisha waandishi wa habari kuwa wananchi wamekuwa wakishuku mienendo ya  mwenye jumba hilo kwani huonekana akirejea usiku wa manane.

Alisema walipofika kwenye jumba hilo waliwapata wanaume wawili ambao walikuwa wametumwa kuyapakia magunia hayo kwenye jumba hilo.

Baadhi ya magunia 222 ya bangi yaliyonaswa katika jumba la kifahari eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tunaelewa vyema hawa jamaa ni wa kutumwa lakini bado tunatafuta mwenye mali hiyo ambaye tunashuku amejificha mahali,” alisema Bw Nyange.

Alisema ushirikiano kama huo ukizidi kuendelea bila shaka maovu mengi hayataweza kuonekana katika makazi yao.

Alisema tayari wawili hao wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Ruiru huku uchunguzi bado ukifanywa ili kubainisha mwenye mali hiyo ni nani.

Naye diwani wa eneo la kahawa Sukari, Bw Livingstone Waiganjo, aliwapongeza wananchi kwa kazi njema waliyofanya kwa sababu ya ushirikiano mwema na Polisi.

“Mimi nasisistiza wananchi wazidi kukumbatia maswala ya Nyumba kumi ambayo ndiyo itaweza kuzuia maovu mengi yanayoshuhudiwa kila mara,” alisema Bw Waiganjo.

Alisema Polisi kwa ujasiri wao pamoja na wananchi walivamia jumba hilo na kugundua biashara haramu ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa njia isiyo halali.

Alisema walanguzi wa bangi wanataka kuharibu vijana na serikali haiwezi kukubali kitendo kama hicho kuendelea miongoni mwa wananchi.

Habari zinazohusiana na hii