Tenisi: Zayyan aingia fainali ya Nairobi Open, ndiye mvulana wa kwanza tangu 2022
KWA mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu, mvulana kutoka Kenya atashiriki fainali ya mchezaji mmoja kila upande katika mashindano ya kiwango cha juu ya Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18.
Zayyan Virani, 16, alifuzu kucheza fainali ya Nairobi Open I (J30 Nairobi) baada ya kupepeta Hursh Patel kutoka India kwa seti 7-5, 6-2 katika nusu-fainali iliyochezewa uga wa Nairobi Club, Ijumaa.
Ni fainali ya kwanza kabisa ya Virani katika ngazi hii. Akiwa ameorodheshwa wa tatu kwenye mashindano hayo ya wiki moja yaliyoanza Juni 30, Zayyan atakutana na Mjerumani Vincent Visker – ambaye hakuwa miongoni mwa wachezaji walioorodheshwa katika 16-bora – katika fainali Jumamosi.
Visker alimduwaza nambari nne kwa ubora, Moeketsi Mokete kutoka Afrika Kusini, seti 7-6, 6-2 kwenye nusu-fainali nyingine.

Virani alianza kucheza tenisi akiwa na umri wa miaka miwili tu na ameonyesha uwezo mkubwa kutinga fainali.
Hakupata mpinzani katika raundi ya kwanza, akambwaga Aarav Dhekial kutoka India 6-2, 6-3 raundi ya pili na kumnyamazisha Hayden Majumdar-Moreau (Canada) 6-0, 6-0 katika raundi ya tatu.
Kisha akampiku Mfaransa Louis Collos 7-6, 7-6 kwenye robo-fainali ya kusisimua kabla ya kumzidia Patel maarifa nusu-fainali.
Kufikia Juni 30, 2025 Virani anashikilia nafasi ya 960 kwenye viwango vya vijana vya ITF, huku kiwango chake cha juu zaidi ambacho amewahi kufikia kikiwa nafasi ya 793 mnamo Februari 17, 2025.
Visker, 15, kwa sasa yuko nafasi ya 3,886 huku kiwango chake bora amewahi kufikia kikiwa nafasi ya 3,810 mapema Juni mwaka huu.
Safari ya Visker kuelekea fainali pia imekuwa ya kuvutia. Alianza kwa kumpiga Mkenya Ruhan Bhandari 6-2, 6-1, kisha akawapepeta Marinos Karniatis (Ugiriki) 6-2, 6-0, Navya Yadav (India) 6-4, 6-4, Gabriel Amengual (Uhispania) 6-1, 6-1, na baadaye Mokete katika nusu-fainali.
Taji la tenisi
Mkenya wa mwisho kufikia fainali ya ITF kwa wavulana katika tenisi ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 alikuwa Kael Shalin Shah, ambaye alipoteza kwa Mhispania Albert Pedrico seti 6-3, 7-6 mashindano ya J4 Les Franqueses del Valles nchini Uhispania mnamo Mei 2022.
Mkenya wa mwisho kushinda taji la ITF la mchezaji mmoja mmoja ni Albert Njogu, aliyemcharaza Abdoul Shakur Kabura kutoka Burundi kwa seti 7-5, 6-1 mashindano ya J5 Nairobi mnamo Julai 2019.
Katika upande wa wasichana, mchezaji wa tano kwa ubora Stacy Yego alifika mbali zaidi kwa kufuzu robo-fainali, ambako alipoteza 6-2, 7-5 mikononi mwa Mwitaliano Chiara Volante.
Washiriki wengine wa Kenya — Liya Gikunda, Jenerica Thuku, Tatiana Gikang’ah, Seline Ahoya, Inaaya Virani, Daniella Muna, na Tumelo Kimunya — walibanduliwa katika raundi ya kwanza huku Nancy Kawira na Sekele Kahi wakiondolewa raundi ya pili.
Yego, Kawira, na Ahoya ni sehemu ya kikosi cha muda cha Kenya kitakachoshiriki Kombe la Afrika la Billie Jean King Cup la Kundi la Tatu nchini Namibia mwezi Agosti.
Timu hiyo pia inajumuisha wachezaji kutoka Amerika; Angella Okutoyi, Cynthia Wanjala, na Alicia Owegi, pamoja na Melissa Mwakha anayeishi Zimbabwe.
Mashindano ya Nairobi Open II (J30 Nairobi II) yamepangwa kuanza Julai 7-12 katika uga huo huo wa Nairobi Club.