Habari za Kitaifa

Boniface Kariuki alivyokata roho baada ya kupambana kwa wiki mbili kusalia hai

Na CECIL ODONGO July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA takribani wiki mbili, alipambana kwa udi na uvumba kuokoa roho roho yake, lakini malaika wa mauti (Izraili) akamtwaa jana alasiri.

Maswali yakiwa yamewajaa kichwani, machozi yakiwatiririsha njia mbilimbili, wingu jeusi likiwatandia, jamaa wa Boniface Kariuki walilemewa na huzuni usiomithilika baada ya kubaini kuwa mwanao alikuwa amewatoka.

Kifo cha Bw Kariuki, 22, kilitokea saa tisa na robo jana katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) alikokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (sadaruki).

Bw Kariuki, muuzaji wa barakoa ambaye alipigwa risasi wakati wa maandamano ya Juni 17, aliaga dunia hospitalini humo ambako amekuwa akipokea matibabu kwa wiki mbili.

Bw Kariuki alipigwa risasi akiwa amebeba barakoa alizokuwa akiuza karibu na Jumba la Imenti wakati wa maandamano jijini Nairobi.

Maandamano hayo yalikuwa ya kupigania haki kwa familia ya bloga na mwalimu Albert Ojwang ambaye aliuawa kinyama mikononi mwa polisi mwezi uliopita.

Bw Kariuki alipigwa risasi kichwani na kuachwa katika hali hatari. Madaktari wamekuwa wakipambana kuyaokoa maisha yake huku kipande cha risasi kikiwa bado kimekwama kwenye ubongo wake.

Mnamo Jumapili, madaktari wa Kenyatta walikuwa wamethibitisha kuwa ubongo wake ulikuwa umekufa huku akipambania uhai wake kutokana na mpigo wa moyo uliokuwa hafifu.

Maafisa wawili wa polisi ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji yake, wanaendelea kuzuiliwa huku uchunguzi ukiendelezwa na Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA).

Wawili hao, Klinzy Barasa Masinde na Duncan Kiprono wamekuwa wakizuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Capitol Hill kuanzia Juni 19, kwa siku 15.

Hapo jana, Msemaji Emily Wanjira alisema mauti hayo ni pigo kwao huku wakililia haki itendeke kwa mwanao.

“Sisi tunasaka haki wala hatuhitaji chochote kwa sababu hayuko nasi. Serikali imekuwa kimya na sasa tunataka kujua nani atalipa Sh3.6 milioni, nani ni sauti yetu?” akauliza Bi Wanjira.

“Kwa nini serikali haiongei, mbona wamenyamaza, tunaomba tusikilizwe. Mtu aliyekuwa akiuza barakoa bila kushiriki maandamano ili kukimu familia yake, aliuawa akisaka riziki. Hili linasikitisha sana,” akasema.

Familia hiyo ilisema haina chochote mbali na nambari ya Paybill 7682551 ambayo sasa wanaomba Wakenya waisaidie kusaka pesa za kulipia bili ya hospitali.

Kufikia Jumatatu jioni, serikali haikuwa imeweka wazi iwapo itafutilia mbali gharama hiyo ya kimatibabu au la.

Jonah Kariuki, babake marehemu alisema kuwa wanaomba usaidizi wa kifedha kwa sababu hawana chochote.

“Tutaanza kupanga mazishi kulingana na vile tutashikiliwa. Mwili umepelekwa mochari na mimi kama babaye, haki pekee kwangu ni kuwa waliomuua mtoto wangu waadhibiwe,” akasema Bw Jonah.

“Sina mtoto mwengine mvulana kwa sababu hao wengine ni wasichana. Sijalala nikiuliza mtoto wangu aliuawa kwa nini? Malezi hayo yote sasa hayana maana kama mwanangu ameuawa hivi,” akaongeza.

Rosemary Njeri, shangaziye marehemu, alilemewa na hisia huku akisisitiza kuwa haki lazima ipatikane kwa vyovyote vile.

Eunice Kiragu, nyanya yake Bw Kariuki naye alishutumu usimamizi wa hospitali ya Kenyatta kwa kuwahadaa na kuwapa matumaini ilhali walijua mwanao hakuwa na nafasi ya kupona.

“Walijua tu hangenusurika lakini hatujui kwa nini walituzungusha. Siku nyingine hata kama ni kufuata utaratibu wa kitaaluma, wangetuambia tu kwa sababu kilio kingekuwa hiki hiki cha leo,” akasema Bi Kiragu.

Ajuza huyo aliwashukuru Wakenya kwa kusimama na familia hiyo na karibu awalaani waliomuua Bw Kariuki. Alisisitiza kuwa serikali inastahili kuwasikiza vijana huku akiomba Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) na Idara ya Mahakama wahakikishe Bw Kariuki anapata haki.