Habari za Kitaifa

Viongozi wa Kiislamu wakosoa mahakama kuruhusu mtoto wa nje ya ndoa kurithi mali

Na MISHI GONGO July 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa Kiislamu mjini Mombasa wamekosoa uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kumpa haki ya urithi mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa, wakisema kuwa hatua hiyo ni kinyume na mafundisho ya sheria ya Kiislamu (Shariah).

Wakizungumza Jumanne nje ya Msikiti wa Sakina baada ya swala ya adhuhuri, viongozi hao walisema uamuzi huo unakiuka misingi ya dini ya Kiislamu na unadunisha mamlaka ya Mahakama ya Kadhi.

Wakiongozwa na Bw Athman Sheriff, ambaye ni miongoni mwa wanaharakati wanaolinda mila na maadili ya jamii, walisema uamuzi huo unafaa ubatilishwe mara moja.

“Masuala ya urithi, ndoa na talaka yanapaswa kushughulikiwa na Mahakama ya Kadhi pekee kwa sababu hiyo ndiyo mahakama inayotambua na kufuata sheria ya Kiislamu. Uamuzi huu unadhoofisha mamlaka ya Mahakama ya Kadhi,” alisema Bw Sheriff.

Kwa upande wake, Sheikh Abu Katada ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Viongozi wa Kidini wa Pwani Wazalendo, alisema walishangazwa na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu, na kwamba suala hilo linapaswa kuachiwa Mahakama ya Kadhi ambayo inaelewa sheria ya Kiislamu.

“Uamuzi huu umeionyesha Mahakama ya Kadhi kama kivuli kisicho na mamlaka yoyote. Tunataka uamuzi huo upitiwe upya kwa sababu hauendani na mafundisho ya dini yetu,” alisema Sheikh Katada.

Walisema kuwa, kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hana haki ya kurithi mali ya baba. Hata hivyo, sheria hiyo haimzuii baba kumlea mtoto huyo kwa kumpa elimu na zawadi wakati wa uhai wake.

“Qur’an iliteremshwa zaidi ya miaka 1,400 iliyopita na imeweka wazi kila jambo. Haiwezi kupingwa wala kubadilishwa,” alisema Bw Mbarak Masoud.

Naye mwanaharakati Abu Muhsin alisema kuwa Mahakama ya Juu imevuka mipaka na wanapaswa kuondoa uamuzi huo mara moja.

Alionya kuwa watakusanya sahihi za wapiga kura milioni moja kupinga majaji waliohusika ili kuhakikisha kuwa masuala ya Kiislamu yanashughulikiwa na Mahakama ya Kadhi pekee.

“Kwa nini tuwe na Mahakama ya Kadhi ikiwa inaweza kupingwa na Mahakama ya Juu? Kuna baadhi ya mambo katika Uislamu ambayo hayapaswi kuguswa. Hii ni hatua yetu ya kwanza kuwasilisha ujumbe kwa Mahakama ya Juu kwamba wamevuka mipaka. Katiba haiwezi kuishinda Qur’an,” aliongeza Bw Muhsin.

Viongozi hao walitoa wito kwa serikali na wadau wa sheria kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.

Waliwataka Mwanasheria Mkuu, Kadhi Mkuu, Chama cha Wanasheria (LSK) pamoja na Baraza la Maimamu na Maulamaa kuingilia kati na kuanzisha mchakato wa kisheria wa kupitia na kupinga uamuzi huo, ili kuhakikisha kwamba misingi ya Kiislamu inalindwa katika masuala ya sheria binafsi yanayowahusu Waislamu.

“Tunatoa wito kwa wabunge, maseneta na magavana Waislamu kujitokeza hadharani na kutetea haki zetu za kikatiba. Tunawasihi waandae hoja bungeni au marekebisho ya sheria yatakayothibitisha uhuru kamili wa Mahakama ya Kadhi kushughulikia masuala ya sheria binafsi za Kiislamu,” walisema viongozi hao.

Waliongeza kuwa wanahitaji sheria ya wazi itakayozuia kuingiliwa kwa maamuzi ya kidini na mahakama za kiraia.

Tayari wameanza kukusanya sahihi kutoka kwa Waislamu kote nchini ili kuwasilisha ombi rasmi kwa Bunge la Kitaifa na Seneti, likitaka uamuzi huo ubatilishwe na sheria maalum zipitishwe kulinda mamlaka ya Mahakama ya Kadhi.

“Uamuzi huu unaonesha kutokuwepo kwa uelewa na heshima kwa sheria ya Kiislamu kutoka kwa baadhi ya wahusika wa mahakama. Hatupingi uadilifu wa mahakama, bali tunasisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya kidini inayolindwa na katiba yetu. Hatuwezi kuruhusu maadili yetu ya kidini kudunishwa na maamuzi yanayopuuza imani yetu na mifumo ya kisheria ya dini yetu,” waliongeza.