Familia ya Ojwang yakana kupokea mchango wa Sh10 milioni
FAMILIA ya mwanablogu marehemu Albert Ojwang’ imekanusha madai yanayoenea mitandaoni kuwa ilipokea Sh 10 milioni kutoka kwa mtu mmoja, ikisema kuwa habari hizo ni za kupotosha.
Akizungumza katika ibada ya wafu ya Ojwang’ iliyofanyika katika kanisa la Ridgeways Baptist Church mnamo Alhamisi, Julai 2, wakili wa familia hiyo, Julius Juma, alieleza kuwa kiasi halisi cha fedha walizopokea ni kidogo ikilinganishwa na kilichodaiwa.
“Imesemekana katika vyombo mbalimbali vya habari kwamba Mzee alipokea Sh10 milioni. Nimetumwa kuweka hili sawa, na nafanya hivyo sasa kutoka madhabahuni,” alisema Bw Juma mbele ya waombolezaji.
Kwa mujibu wa wakili huyo, jumla ya michango ya fedha iliyopokewa na familia ya Ojwang’ ni Sh5.6 milioni zinazojumuisha Sh2 milioni kutoka kwa Rais William Ruto, Sh1 milioni 1 kutoka kwa Kiongozi wa ODM Raila Odinga, na Sh2.6 milioni kutoka kwa wananchi wa kawaida, waliotoa kati ya shilingi moja na mia moja.
“Tunaweka rekodi sawa kwa heshima ya familia na umma unaoumia pamoja nasi,” alisisitiza Bw Juma.
Marehemu Ojwang’ alifariki dunia katika mazingira tata mnamo Juni 8 na kifo chake kilizua hasira na maandamano kote nchini, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi cha Gen Z.
Familia pia imekumbwa na shinikizo mitandaoni, hasa baada ya kudaiwa kuwa baba yake Ojwang’ alipokea simu ya moja kwa moja kutoka kwa Rais.
Mnamo Juni 24, msemaji wa familia alikanusha madai kwamba pesa zote zilipatikana kutoka kwa michango ya wananchi pekee.
Ojwang’ anatarajiwa kuzikwa Julai 4 katika kijiji cha Kakwonyo, Kaunti ya Homa Bay, nyumbani kwa baba yake.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameidhinishwa mashtaka ya mauaji dhidi ya OCPD wa kituo cha polisi cha Nairobi Central , Samson Talaam, pamoja na konstebo James Mukhwana, Konstebo Peter Kimani na washukiwa wengine.