Habari

Ojwang azikwa, LSK kuteua mawakili zaidi kutafutia familia haki

Na MARY WANGARI July 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA ya Albert Ojwang itashirikisha timu ya mawakili na wataalam wa sheria kwenye kesi inayohusisha polisi na kifo chake katika juhudi za kupata haki.Wakili wa familia, Julius Juma, amesema huduma ya kisheria itafadhiliwa na Chama cha Mawakili Nchini (LSK).

Alisema rais wa LSK Faith Odhiambo atatuma mawakili mbalimbali kortini tarehe tofauti kujaribu kuishawishi mahakama kuwahukumu washukiwa katika kesi hiyo.

“Tulikuwa na mawakili wanne wiki iliyopita. Wengine watakuja kortini tarehe tofauti tofauti kuanzia wiki ijayo,” alisema.

Bw Juma ambaye amewakilisha familia hiyo tangu mwana wao alipokamatwa mwezi uliopita hakutaja atakayemsaidia katika shughuli hiyo ya kisheria. ‘LSK ina maelfu ya mawakili.

Yeyote miongoni mwao anaweza kutumwa kortini,” alieleza Taifa Leo.

Bw Juma alitoa wito kwa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (Ipoa) kufanya hima kukamilisha uchunguzi ili kesi ianze.

Alisema Ipoa imeashiria haijakamilisha uchunguzi.

“Sitakua pekee yangu ila nitasaidiwa na LSK kuhakikisha watu waliohusika na kifo hicho wanakabiliwa kisheria kikamilifu. Tutahakikisha kila mmoja, pasipo kujali hadhi yao, wanakabiliwa kikamilifu kisheria,” alisema.

Ojwang alizikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Kakoth, Kabondo Kasipul, jana katika hafla iliyohudhuriwa na vijana ikiwemo walimu, wanafunzi wa chuo kikuu na wanasiasa.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa ODM Nchini, Gladys Wanga, Kiranja wa Wachache, Millie Odhiambo, wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Eve Obara (Kabondo Kasipul) na Mwakilishi Mwanamke Homa BayJoyce Osogo, wanasiasa walitaka haki kwa familia ya marehemu.

Bi Wanga alisema kinara wa ODM Raila Odinga aliyetarajiwa kusafiri Homabay hakuhudhuria mazishi kutokana na sababu zilizomzuia.

“Nimeleta ujumbe wa rambirambi zake kinara wa chama chetu na Rais William Ruto,” alisema Bi Wanga.Mbunge wa Suba Kaskazini alikemea kifo cha Ojwang akiwarai Wakenya kuungana licha ya kinachotendeka nchini.

“Mambo mengi huunganisha taifa. Kifo hiki kituunganishe na kuhakikisha hakuna yeyote atakayekumbana na kifo kama hiki,” alisema Bi Odhiambo.