Habari

‘Kisumu tunapunga hewa nzuri’: Hakuna maandamano Nyanza

Na DOMNIC OMBOK July 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAUNTI za Nyanza Jumatatu zilishuhudia utulivu mkubwa wakati wa maandamano ya Saba Saba huku fujo na makabiliano yakiripotiwa maeneo mengine.

Japo shule nyingi zilifungwa jijini Kisumu wazazi wakichukua tahadhari, biashara zilinoga Kisumu bila tatizo lolote.

Kati ya maeneo ambayo yalishuhudia utulivu mkubwa yalikuwa katikati mwa jiji la Kisumu, Nyalenda, Nyamasaria huku biashara nyingi zikifunguliwa.

Awali wafanyabiashara na wakazi walisema hawataki maandamano hayo wakisema yanachochewa kisiasa na yanalenga kulemaza njia yao ya kujizimbulia riziki.

“Hatutaki maandamano hapo kwa sababu sisi tumeamua kukumbatia amani na tutaendelea hivyo,” akasema Mhudumu wa bodaboda Austin Ochieng’.

Marseline Wasonga, mfanyabiashara katika soko la Kibuye alisema maendeleo ambayo Kisumu imeyapata katika utawala huu hayawezi kufanya waandamane kuitikia wito wa mrengo mwingine wa kisiasa.

“Kisumu ilikuwa kitovu cha maandamano lakini tulishuhudia uharibifu mkubwa wa mali, kupotea kwa ajira na sifa mbaya. Tangu tuache maandamano, maendeleo yanatufuata tu,” akasema Bi Wasonga.

“Hata watu kutoka maeneo mengine wanakuja kusoma na kujifunza maendeleo kutoka kwetu. Tuandamane kwa sababu gani?” akauliza mfanyabiashara huyo huku akiwahudumia wateja.

Hii ni mara ya pili Kisumu ilisusia maandamano baada ya kuwafukuza waliojaribu kuandamana jijini humo mnamo Juni 25 wakati wa kuadhimisha mwaka moja ya mauaji ya Gen Z.

Polisi hawakuonekana kuwa na shughuli jijini humo, wachache tu wakipiga doria huku wakishangiliwa na wakazi.

Kamishina wa Kaunti ya Kisumu Benson Leparmorijo awali alikuwa ametoa wito wa amani na kuwataka wafanyabiashara waendelee na kazi zao kama kawaida.

Aidha maandamano hayakushuhudiwa kaunti nyingine za Nyanza isipokuwa madogo Kisii huku kaunti za Magharibi mwa nchi pia zikishuhudia utulivu.