Habari

Ruto, Koome na Duale waongoza umma kuomboleza kifo cha Kadhi Mkuu Sheikh Hussein

Na CHARLES WASONGA July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome wamewaongoza viongozi nchini kuomboleza kifo cha Kadhi Mkuu Sheikh Athman Abdulhalim Hussein aliyefariki Alhamisi, Julai 10, 2025 alfajiri akiwa Mombasa.

Kwenye risala yake aliyotoa Alhamisi asubuhi, Dkt Ruto alimtaja Sheikh Abdulhalim kama kiongozi aliyejitolea kuhudumia umma na aliongoza jamii ya Kiislamu kwa “unyenyekevu, hekima na moyo wa kujitolea.”

Rais alisema mwendazake atakumbukwa kama Msomi Mkuu wa Kiislamu aliyejitolea kutenda na kuendeleza haki.

“Naungana na jamii ya Kiislamu kuomboleza kifo cha Kadhi Mkuu Sheikh Abdulhalim Hussein.

“Tunaomba kwamba Allah aifariji familia yake na jamii yote ya Kiislamu wakati huu wa majonzi,” akaeleza Dkt Ruto.

Kifo cha Kadhi Mkuu kilitangazwa Nairobi Alhamisi, Julai 10, 2025 na Sheikh Jamaludin Osma, Imam wa Msikiti wa Jamia.

“Nahuzunika kuwaatifu kuhusu kifo cha Kadhi wetu Mkuu Sheikh Abdulhalim Hussien, muda mfupi uliopita akiwa Mombasa.

“Atazikwa Mombasa,” Sheikh Osman akaongeza.

Kwenye ujumbe wake, Jaji Mkuu Koome alimtaja Kadhi Mkuu kama kiongozi aliyejitolea kutoa haki, kukuza na kuendeleza sheria za kiislamu na kuelekeza jamii kimaadili.

“Uongozi wake, unyenyekevu, kujitolea kwake kudumisha utawala wa kisheria na yaliyomo kwenye Katiba yetu kanuni za kiislamu utakumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo,” akaeleza.

“Tunakumbuka na kuthamini mchango mkubwa wa Sheikh Abdulhalim kwa Idara ya Mahakama na katika uendelezaji wa masuala ya kiroho na kisheria nchini mwetu,” akaongeza Jaji Mkuu Koome.

Naye Waziri wa Afya Aden Duale alimtaja kama kiongozi, ndugu na msomi mashuhuri.

“Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un. (Sisi wote ni wa Allah, na kwake tutarejea)

Kufuatia kifo cha msomi wetu, ndugu na kiongozi wa kidini, Kadhi Mkuu wa Kenya, Ndugu Abdulhalim Hussein, jijini Mombasa,” akaeleza kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa X.

Chanzo cha kifo cha Sheikh Athman Abdulhalim Hussein hakikufichuliwa mara moja ingawa vyanzo vya familia vilisema alikuwa akiugua kwa muda.

“Alikuwa kiongozi mnyenyekevu na kielelezo kwa wengi kimazungumzo na kivitendo,” Bw Duale akaongeza.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir pia alimwomboleza marehemu Hussein akimsifu kwa huduma zake kwa jamii ya Kiislamu nchini Kenya.

“Nimehuzunishwa sana na kifo cha Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim Hussein. Kwa hakika sisi sote ni watoto wa Allah na kwake tutarejea,” akasema.

Gavana Nassir akaongeza: “Allah amsamehe, aongeze manufaa ya matendo yake mazuri kwa umma wa Waislamu na ampe hadhi ya juu zaidi ya Paradiso.”

Mwendazake aliteuliwa Kadhi Mkuu na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo Julai 2023 baada ya kuibuka bora zaidi miongoni mwa wawaniaji watano wa nafasi hiyo.

Sheikh Abdulhalim alijaza nafasi ya Sheikh Ahmed Muhdhar, aliyestaafu baada ya kuhudumu kwa miaka 12 na kutimu umri hitajika wa miaka 60.

Mahakama za Kadhi nchini hutekeleza wajibu wa kutoa haki haswa katika masuala yanayohusiana na sheria za Kiislamu

Mahakama hizo husikiza na kuamua kesi zinazohusiana na mizozo ya ndoa, talaka, urithi na masuala mengine ya kifamilia kwa misingi ya Sheria ya Kiislamu.