Kimataifa

Trump asifu Rais wa Liberia kwa ufasaha wa Kiingereza

Na REUTERS July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WASHINGTON, AMERIKA

KATIKA tukio nadra sana, Rais wa Amerika Donald Trump amemsifia kiongozi wa Afrika kwa kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.

Trump mnamo Jumatano alikutana na kundi la marais kutoka Afrika ambao wanazungumza lugha mbalimbali.

Walitumia nafasi hiyo kutoa wito wa kukuzwa kwa uhusiano wa kibiashara kati ya Amerika na nchi zao.

Hata hivyo, kilichomteka makini Trump ni jinsi Rais wa Liberia Joseph Boakai alivyozungumza Kingereza kwa ufasaha akipigia debe kuimarishwa kwa uhusiano kati ya taifa lake na Amerika.

“Liberia ni rafiki mkubwa wa Amerika na tunaamini katika sera yako ya kufanya Amerika iwe bora tena (MAGA),” akasema Rais Boakai kwenye Ikulu ya White House wakati wa mkutano huo wa uwekezaji na marais wa Guinea Bissau, Senegal, Mauritania, Gabon na Liberia.

“Tunataka kukushukuru sana kwa nafasi hii tukizi ya kukutana nasi,” akaongeza.

Trump alifurahishwa na ufasaha wa Boakai hata akauliza mahali ambapo kiongozi huyo alisomea lugha.

“Kingereza kizuri na bora zaidi. Ulisoma wapi? Unazungumza kwa njia ya kupendeza na kwa ufasaha wa kupigiwa mfano,” akasema Trump.

“Ulisomea Liberia?” akauliza Trump.

Boakai alimjibu kuwa alisomea Liberia huku akionekana kutabasamu na wakati huo huo kushangazwa na pongezi za Trump kwa kuwa hakuzitarajia.

“Hivyo ni vizuri sana. Nina watu kwenye meza hii ambao hawawezi kuzungumza kwa ufasaha kwa Kingereza kizuru jinsi unavyofanya,” akaongeza Trump.

Liberia ni nchi ambayo ilianzishwa mnamo 1822 baada ya kuwa chini ya utawala wa Waamerika.

Kingereza ndiyo lugha rasmi ya raia nchini Liberia japo lugha nyingine za asili huzungumzwa pia nchini humo.