Afisa wa kaunti asema gatuzi liko ange kupambana na majanga
AFISA wa Kaunti ya Nairobi anayesimamia idara ya kupambana na majanga ya dharura Bramwel Simiyu amekanusha madai kuwa wamekuwa wakilemewa kupambana na visa vya moto katika mitaa ya mabanda.
Bw Simiyu alikiri kuwa japo kuna changamoto ibuka wakati wa kupambana na majanga, kaunti hiyo imekuwa ikifanya kila juhudi kufanikisha uokoaji wa mali na maisha ya raia.
“Binafsi nimekuwa nikifanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa kaunti hii inafanya juu chini kukabiliana na majanga mbalimbali ya dharura kote jijini,” akasema Bw Simiyu.
Alitaja mitaa ya mabanda kama Kibra, Mathare, Korogocho na Mukuru kama inayoshuhudia visa vingi vya moto lakini kaunti hiyo hupambana kuhakikisha juhudi za uokoaji zinafanikiwa.
Ili kuimarisha utendakazi wake na jinsi visa vya dharura vinavyokabiliwa, afisa huyo alisema Kaunti itakuwa ikiendeleza hamasisho kwa raia.
“Wafahamu kuwa wanastahili kupiga simu kwa wanaosimamia zimamoto kwenye nambari zinazofahamika na pia wahakikishe usalama wao na walioathirika,” akasema Bw Simiyu. Kaunti pia inapanga kujenga kituo cha kuzima moto katika soko la Gikomba.
Mwanakandarasi yupo kwenye hatua za mwisho mwisho katika maandalizi yake kabla ya uzinduzi kufanyika kwa mujibu wa Bw Simiyu.
Mradi wa kujenga kituo hicho cha moto ni kati ya miradi ambayo Gavana Johnson Sakaja aliahidi alipochukua mamlaka pamoja na kujenga soko la kisasa.