Habari za Kitaifa

Ushindi kwa vijana Fahima, 33, akitwaa kiti cha naibu bosi wa IEBC

Na CHARLES WASONGA July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NI ushindi kwa vijana barobaro nchini kufuatia kuchaguliwa kwa Fahima Araphat Abdallah kuwa naibu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kwenye taarifa aliyotoa jana jioni, mwenyekiti mpya wa tume hiyo Erustus Edung Ethekon alisema kuwa Bi Abdallah, mwenye umri wa miaka 33, alichaguliwa kwenye kikao cha 228 cha makamishna wa IEBC saa chache baada ya kuapishwa kwao.

“Baada ya kuapishwa kwa Mwenyekiti na Makamishna wa tume hii, ni furaha yetu kutangazia umma na wadau kwamba makamishna katika kikao rasmi cha 288 walimchagua Kamishna Fahima Araphat Abdallah kuwa Naibu Mwenyekiti wa tume,” akasema.

“Akaongeza: “Tume inachukua nafasi hii kumpongeza Kamishna Fahima kwa kuchaguliwa kwake.”

Kwa kuchagua naibu mwenyekiti saa chache baada ya kuapishwa kwao, Bw Ethekon na wenzake wameonyesha ari ya kuanza kutekeleza majukumu yao kikatiba pasina kupoteza wakati.

Majukumu hayo ni kama vile kuandaa chaguzi ndogo katika maeneo 22 ya uwakilishi, yakiwemo maeneo bunge, wadi na kaunti ya Baringo ambako nafasi ya Seneta iko wazi.

Aidha, Bw Ethekon na wenzake wataanzisha upya shughuli ya usajili wa wapiga kura na uchoraji upya wa mipaka ya maeneo  ya uwakilishi.

Kuchaguliwa kwa Bi Fahima kuwa naibu mwenyekiti wa IEBC kunatarajiwa kuwavutia vijana wengi watakuwa na ari ya kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuwa wapiga kura wakati kama huu ambapo wameonyesha kuchoshwa na utawala wa sasa.

Makamishna wengine wa IEBC walioapishwa jana ni pamoja na Bi Anne Nderitu, Moses Mukhwana, Bi Mary Sorobit, Profesa Francis Aduol na Bw Hassan Noor Hassan.