Habari za Kitaifa

Msije kwa meza bila pesa, Kuppet yaonya TSC kuhusu mazungumzo ya mishahara

Na  LYNET IGADWAH July 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo vya Kati (KUPPET) kimetahadharisha Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) dhidi ya kuwasilisha pendekezo la makubaliano ya pamoja ya 2025–2029 (CBA) lisilo na faida za kifedha, kikisisitiza kuwa walimu wanataka pesa moja kwa moja.

Haya yanajiri wakati TSC ikiomba muda zaidi kushauriana na taasisi nyingine za serikali kabla ya kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu CBA mpya, licha ya kumalizika kwa makubaliano ya awali Juni 30, ambayo yalikuwa yameanza kutekelezwa tangu 2021.

Akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa KUPPET, Bw Akelo Misori, alisema wanachama wa chama hicho wameanza kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kucheleweshwa kwa majibu ya TSC, akisisitiza kuwa pendekezo lolote linalokubalika lazima lijumuishe faida ya kifedha moja kwa moja.

“TSC ifichue pendekezo lake la pili kwa sababu kuchelewa huku kunazua wasiwasi mkubwa. Uchumi umeimarika na mfumuko wa bei umepungua, sasa walimu wanataka pesa mikononi mwao na mifukoni mwao,” alisema Bw Misori.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa KUPPET, Bw Omboko Milemba, alikumbusha TSC kuhusu upinzani mkubwa uliokuwepo kufuatia makubaliano ya 2021–2025 ambayo yalikuwa hayana faida ya moja kwa moja ya kifedha wakati wa janga la Covid-19.

“Wanachama wetu wametuonya tusikubali makubaliano kama hayo tena. Safari hii tunasisitiza kuwe na ahadi madhubuti za kifedha,” alisema Bw Milemba.

KUPPET imewasilisha mapendekezo mbalimbali kwa TSC, ikidai nyongeza ya mishahara ya asilimia 30–70 na ongezeko la asilimia 100 kwa baadhi ya marupurupu.

Chama hicho pia kinataka muda wa mizunguko ya makubaliano upunguzwe kutoka miaka minne ya sasa hadi miaka miwili, ili kuruhusu marekebisho ya haraka ya mishahara.

Aidha, chama hicho kinataka tathmini mpya ya maelezo ya kazi za walimu wa kawaida darasani, kikidai kuwa muundo wa sasa unawapendelea zaidi wasimamizi wa shule, licha ya wanachama wao kuwa na sifa na uzoefu sawa.

Katika mapitio yaliyopita, Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) iliwatambua wasimamizi kama viongozi, jambo lililosababisha pengo kubwa la mishahara kati ya wasimamizi na walimu wa kawaida.

Miongoni mwa hoja kuu zilizowasilishwa ni kuhusu Mwongozo wa Ukuaji wa Kitaaluma ambao KUPPET inataka uondolewe ili walimu waweze kupandishwa cheo wa moja kwa moja hadi ngazi ya Naibu Mwalimu Mkuu.

KUPPET pia inataka kuondolewa kwa nyadhifa za ‘kaimu’ zisizolipwa, na inataka walimu zaidi ya 99,000 wanaoshikilia nyadhifa hizo kwa sasa walipwe mshahara wa kamili wa majukumu.