Ujanja wa Raila kuzima Gen Z
PENDEKEZO la kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuhusu kongamano la mdahalo kukutanisha vijana na tabaka la wanasiasa wakongwe limeibua mjadala mkubwa na hata hofu kutoka kwa baadhi ya viongozi wa siasa na wataalamu wa utawala.
Wataalamu wa utawala na wachanganuzi wa siasa wanahisi kuwa wanasiasa wa sasa hawana nia njema kuhusu pendekezo hilo na hawataki mabadiliko wanayopigania vijana na hii huenda ikazima juhudi zozote za kutatua mzozo uliopo kwa sasa hasa ikiwa Raila ataendelea kushirikiana na utawala wa Kenya Kwanza.
Aliyekuwa karani wa Baraza la Jiji la Nairobi na mtaalamu wa utawala, Philip Kisia anasisitiza kuwa ingawa mazungumzo ni muhimu, ni vema kuweka masharti madhubuti kabla ya kuanzishwa kwake.
Kisia anasema kuwa ukweli na uaminifu vinapaswa kuwa nguzo kuu za mazungumzo haya, na kwamba lazima kuwe na dhamira thabiti ya kutekeleza matokeo yatakayopatikana ili kuepuka hatari ya tabaka fulani la wanasiasa kudhibiti taifa kwa masilahi yao binafsi.
“Kuna vitu viwili vikubwa vinavyopaswa kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa mazungumzo haya. Kwanza, ukweli unapaswa kuwekwa mezani; na pili, uaminifu unapaswa kuwekwa mezani. Bila haya na dhamira thabiti ya kutekeleza matokeo, hatutaepuka hatari ya tabaka fulani la wanasiasa na serikali kudhibiti taifa kwa maslahi yao binafsi,” Kisia alisisitiza.
Aliongeza kuwa bila tahadhari hizo, kuna hatari kubwa ya mazungumzo haya kugeuka kuwa jukwaa la kuendeleza hali ya sasa, badala ya kuleta mabadiliko makubwa yanayohitajika katika maisha ya Wakenya wa kawaida.
Kisia pia alisisitiza kuwa lazima kuwe na mifumo ya kuzuia mazungumzo haya kugeuka kuwa malumbano yasiyo na faida.
“Tunapaswa kujiuliza ni tahadhari gani tumekuwa nazo kuhakikisha mazungumzo haya yana maana, na yataleta matokeo yanayotarajiwa, kuepuka kutekwa na tabaka fulani la wanasiasa au serikali, na kuepuka kuongozwa na tabaka hilo? Kwa sababu hawa watu wana ajenda moja tu; ni tabaka lile lile, hawawezi kuhimili mabadiliko,” aliongeza Kisia.
Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, amemshauri Raila Odinga kuondoa ushirikiano wake wa kisiasa kwa Rais William Ruto kupitia Serikali Jumuishi, akisema kuwa Kenya inahitaji mabadiliko ya kweli na mageuzi makuu.
Katika chapisho katika mitandao yake ya kijamii Ijumaa, Amisi alisema kuwa wito wa Raila wa kuandaa kongamano la kitaifa unahitaji kuongozwa na viongozi wenye maadili na busara, na si wale wanaohusiana moja kwa moja na serikali ya sasa.
Amisi alisisitiza kuwa Raila hana deni kwa mtu yeyote, na kwamba kama atachukua hatua ya kuachana na serikali ya Rais Ruto, basi atahifadhi hadhi yake ya kiongozi wa taifa na kudumisha heshima yake katika siasa za Kenya.
“Baba mpendwa Raila Odinga, kiongozi wangu wa Orange Democratic Movement (ODM), unajua heshima yangu kwako ni kubwa sana, na ni kwa sababu umeonyesha kuwa mpiganiaji wa haki na maendeleo kwa Wakenya. Njia bora ya kuendesha mazungumzo haya ni kwa kuondoa wanachama wa ODM walioko serikali na kuungana nasi katika kuondoa Kasongo,” alisema Amisi.
Amisi alidai kuwa Rais William Ruto amesababisha madhara makubwa kwa taifa, na yeye pamoja na marafiki zake hawajali madhara hayo. Alisema kuwa Ruto na kundi lake hawajasikiliza wito wa Wakenya na hawawezi kuleta mabadiliko chanya yanayohitajika.
Mbunge huyo alibainisha kuwa makubaliano ya kisiasa kati ya Raila na marais wa zamani yamekuwa na athari mseto, lakini makubaliano ya sasa na Rais Ruto yataweza kuwa pigo kubwa na yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa amani na utulivu wa taifa.
Mnamo Mei 2025, Rais William Ruto na Raila Odinga walitia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) ambayo yaliwezesha chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Ruto na Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila kushirikiana katika serikali.
Makubaliano hayo yaliorodhesha vipengele kumi vya kushughulikia changamoto za taifa kama vile gharama kubwa ya maisha, ufisadi, ukosefu wa ajira, deni kubwa la taifa, haki ya kuandamana kwa amani, kuheshimu katiba na kupunguza matumizi mabaya ya rasilmali.
Wito wa Raila wa kuandaa kongamano la kitaifa umeibua mjadala mkali kuhusu tofauti ya mdahalo huo na iliyofanyika awali bila ripoti kutekelezwa.
“Kwa maoni yangu, ni mbinu ya kuzima harakati za vijana ambazo zinatishia maisha ya kisiasa ya tabaka la watawala na wanasiasa wa miaka mingi ambao hawajali hatima ya vizazi vijavyo,” asema Samuel Ndeto, mchanganuzi wa siasa.