Jinsi ya kuepusha watoto na athari za uraibu wa TikTok, Instagram
MITANDAO ya kijamii kama WhatsApp, Instagram, X na TikTok imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya vijana wengi.
Mitandao hii inaweza kuunganisha watu, lakini pia inaweza kuchangia matatizo ya kiakili na kijamii. Inatoa taarifa muhimu lakini pia inasambaza habari potovu; inaweza kuongeza kujiamini au kudhoofisha hali ya mtu kujihisi vizuri.
Kwa hivyo, haishangazi kwamba suluhisho kwa matatizo yanayosababishwa na mitandao hii inaweza pia kupatikana kupitia mitandao yenyewe.
Watafiti wanasema kwamba wasiwasi wa kijamii au hofu ya kuhukumiwa na watu wengine mara nyingi hutokana na historia ya kushindwa au mtazamo hasi wa mtu binafsi kuhusu yeye mwenyewe. Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba matumizi kupita kiasi ya mitandao ya kijamii huongeza hali hiyo kwa vijana na watu wazima wachanga.
Utafiti
Kwa mfano, utafiti mmoja uliofanywa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini China na mtafiti Li Sun, uligundua kwamba matumizi ya mitandao yalihusishwa na kuongezeka kwa upweke, wasiwasi na kupungua kwa ustawi wa kisaikolojia.
Lakini baada ya kutumia programu ya simu iliyozingatia mbinu za kutuliza akili kwa wiki nane, waliona mabadiliko makubwa. Wanafunzi walipendelea programu hiyo kwa sababu haikuhitaji kukutana na watu moja kwa moja, ilikuwa rahisi kutumia, na ilipunguza aibu ya kutafuta msaada wa kisaikolojia.Watafiti wengine kama Katie Davis pia wanaendeleza mbinu mpya.
Walitengeneza programu inayohamasisha vijana kutafakari kabla ya kufungua mitandao yao ya kijamii. Wanafunzi 66 walipoitumia kwa wiki mbili, waliripoti kuwa na udhibiti bora wa matumizi ya mitandao, walikuwa makini zaidi, na walihisi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi wenyewe.
Hii inaonyesha kuwa teknolojia inaweza kutumika kubadili mitazamo na tabia kuhusu mitandao ya kijamii.Kabla ya kufungua Instagram au TikTok, jiulize: ‘Kwa nini nataka kufungua hii sasa?’ Hili husaidia kuzuia matumizi ya mitandao kwa mazoea tu bila sababu maalum.
Kukabiliana na athari
Chagua kufuata akaunti zinazokuinua kifikra na kihisia. Usisite kuacha kufuata akaunti au watu wanaokuletea msongo wa mawazo au kukuacha ujihisi vibaya.
Vilevile ni muhimu kupanga muda wa kuwa nje ya mitandao ya kijamii. Hata dakika 30 kila siku zinaweza kusaidia akili kupumzika na kuboresha hali yako ya kihisia.Kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya hekima na utulivu wa akili, vijana wanaweza kujikinga dhidi ya athari zake hasi na kuimarisha afya.