Kundi la Gen Z kuandaa tamasha la kuchangisha Sh3.5m za kujenga studio
HUKU taifa likiendelea kuandamwa na ukosefu wa ajira, kundi la vijana kutoka Nairobi wameungana na sasa wanazumbua riziki kupitia usakataji densi.
Kupitia kundi lao ChezaCheza All Stars, vijana hao wa kati ya umri wa miaka 14 na 22 kutoka familia maskini na mitaa ya mabanda wamekuwa wakitumbuiza mashabiki katika maeneo mbalimbali jijini ili kupata riziki na kukuza talanta zao.
Mnamo Agosti 3 kundi hilo limepanga tamasha kubwa ambapo watawasilisha densi yao ‘Eye of the Storm’ katika ukumbi wa Jain Bhavan, Loresho.
Wasilisho hilo linalenga kuhakikisha wanachangisha Sh3.5 milioni kujenga studio ya kisasa ambako zaidi ya vijana 200 watakuwa wakisomea masuala ya muziki na talanta kila mwaka.
Tamasha hiyo pia itaanika masuala ya kijamii na kimazingira kama mabadiliko ya tabianchi, ubaguzi wa kijinsia, dhuluma za kijinsia miongoni mwa changamoto nyingine ambazo watoto wanaoishi mitaa ya mabanda hukumbana nazo.
“Tuko kwenye kizazi ambacho hakipo tayari kusubiri na kinataka uwajibikaji. Hii ndiyo maana kundi hili lipo ili kuwashughulisha vijana wenye talanta ndipo wasizamie uhalifu na maovu mengine,” akasema mkuu wa wakfu wa ChezaCheza Natasha Sifa.
Wengi wa wanachama wa ChezaCheza wanatoka mitaa ya mabanda ya Mathare, Kibra na Kangemi. Nyingi za nyimbo zao na densi wanazosakata hujikita katika kuwaelimisha vijana, masuala ya uongozi na afya yao ya kiakili.