• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
6 kunyongwa kwa kuua na kutupa mwili mtoni

6 kunyongwa kwa kuua na kutupa mwili mtoni

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE aliyeshirikiana na mwanawe, dada yake na wanaume wengine watatu kumuua kinyama mumewe kisha wakafungia mawe mazito kwa maiti hiyo na kuitupa katika maporomoko ya maji Kaunti ya Kiambu miaka 15 iliyopita wamehukumiwa kunyongwa.

Baada ya kumuua David Macharia Juni 12 2004 , Anne Waithera na wauaji hao waliufunga mwili wake kwa blanketi, wakauweka ndani ya gunia na kuusafirisha kwa baiskeli hadi katika msitu wa Kamae/Kinale usiku na kuitupa maiti katika maporomoko ya mto ujulikanao Wagura eneo la Lari kaunti ya Kiambu.

Kabla ya kutumbukizwa mtoni maiti ya Macharia ilifungiwa mawe mawili makubwa na kutupwa mle asiwahi patikana.

Lakini kisa hicho hakikuweza kufichika kama ilivyokusudiwa kwa vile Waithera, mwanawe Joseph Macharia Maina , dada yake (waithera) Ruth Wanjiru Maina,David Njoroge Kimotho, Joseph Kinyuru Kirumbi na Eliud Kimani Mwai walikamatwa na kuelezea polisi walichokitenda kwa siri.

Siri ya mauaji ya Macharia ilitobolewa na Kinyuru alipoenda kujificha kwa mjomba wake eneo la Mai Mahiu akihofia kushikwa na kushtakiwa kwa mauaji ya Macharia.

Mjombawe alipopata habari hizo alifufululiza moja kwa moja hadi kituo cha Polisi na kuwapasha habari na ndipo Kinyuru alitoboa siri jinsi Macharia alivyokatwa kichwa akikamua mifungo wake asubuhi ya Juni 12 2004.

Nduguye Macharia na mke wa pili wa Macharia walikuwa pia wamefanya kila juhudi kumtafuta lakini hawakufanikiwa.

Kinyuru aliwapeleka Polisi hadi kwenye mto wa Wagura na kuwaonyesha mahala alitupa mwili huo akiwa na Kimotho na Mwai.

Polisi waliipata Jaketi katika bafu na upanga uliotumiwa kukata shingo ya Macharia ulikuwa umefichwa chini ya mbao zilizokuwa zimejenga bafu hiyo.

Sita hao walipatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa na Jaji Florence Muchemi mnamo Feburuari 27 2014.

Sita hao walikata rufaa wakisema Jaji Muchemi alikosea sheria kuwahukumu kifo kwa vile hakukuwa na shahidi aliyewaona wakimuua Macharia.

Lakini Majaji Philip Waki, Roselyn Nambuye na Patrick Kiage walitupilia mbali rufaa hiyo wakisema ushahidi uliotolewa ulithibitisha kabisa kwamba ni wao walimuua Macharia.

Majaji hao walisema mvulana mwenye umri wa miaka tisa aliwasikia Waithera , dada yake Ruth na mwanawe Waithera Maina wakisema “lazima Macharia apewe dawa kwa kumtaabisha Mwangi (mwanawe waithera).”

Mvulana huyo alisema alisema Waithera na watu wengune walipanga jinsi ya kumuua Macharia mara kadha hata dada yake Ruth akaenda kukopa pesa kwa Mwai akimdanganya zilikuwa za kulipia mwanawe karo ya shule.

Waithera aliwatafuta Kinyuru na Njoroge kutekeleza mauaji hayo.

Ijapokuwa washtakiwa wote walijitetea hawakuhusika na mauaji hayo , majaji hao hao walisema wenye kupanga njama hiyo (waithera , maina na ruth) , mfadhili (mwai) na wenye kutekeleza mauaji ,kusafirisha mwili na wenye kuutupa usiku wa manane katika maporomoko wote walikuwa na nia moja- kuua.

“Washtakiwa wote sita wako na hatia na rufaa waliyowasilisha kupinga uamuzi wa kuhukumiwa kunyongwa na Jaji Muchemi wafaa,” walisema majaji hao sita.

Majaji hao walisema kufutilia mbali kwa hukumu hiyo ya kifo dhidi ya sita hao ni kuchangia pakubwa kutokomezwa kwa maisha ya marehemu jehanamu

Mahakama ilisema siku hizi maisha ya ndoa yamekuwa chanzo cha wazazi wengi kupoteza maisha yao katika mikono ya watoto wao wasio tazama nyuma wanapoamua kuangamiza maisha ya wazazi wao.

Majaji hao walisema utu umewaondoka wengi na ni lazima sheria itekeleze wajibu wake.

Walisema lazima mahakama ziwaadhibu wahalifu kwa makali na uzito ambao sheria imetangaza.

Majaji hao walisema wauaji sampuli hii hawapasi kuruhusiwa kuendelea kupumua hewa safi na kuruhusiwa kutembea katika nchi ya wapenzi wa amani bali wanatakiwa kutengwa na wastaarabu kwa vile hawathamini maisha.

  • Tags

You can share this post!

Polisi washindwa kueleza jinsi matamshi ya Kuria yangezua...

Ole Gunnar amchemkia Sanchez

adminleo