Aliyekuwa mbunge wa Karachuonyo na mtetezi wa wanawake Asiyo afariki dunia
DAKTARI Phoebe Muga Asiyo, mtetezi maarufu wa haki za wanawake na aliyewahi kuwa Mbunge wa Karachuonyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 huko North Carolina, Amerika, familia yake ilithibitisha Alhamisi, Julai 17, 2025.
“Kwa mioyo iliyojaa huzuni, familia ya Asiyo inatangaza kifo cha mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt Phoebe Muga Asiyo. Upendo wake na uwepo wake vitakumbukwa sana na wote waliomjua,” ilisema familia katika taarifa rasmi. Maelezo kuhusu mipango ya mazishi itatolewa baadaye.
Bi Asiyo atakumbukwa kama sauti isiyotetereka ya wanawake nchini Kenya. Alikuwa Mwenyekiti wa kwanza Mwafrika wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake (MYWO) alipochaguliwa mwaka 1958.
Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Karachuonyo mara mbili—mwaka 1982 na tena 1992—na alitumia nafasi hiyo kuongoza juhudi kubwa za kuendeleza usawa wa kijinsia.
Mwaka 1997, aliwasilisha Hoja ya Utekelezaji wa Usawa bungeni, iliyolenga kusaidia waathiriwa wa dhuluma za nyumbani, wajane waliopokonywa mali, wanawake wanasiasa waliokumbana na vurugu wakati wa uchaguzi, na masuala kama ukeketaji na ndoa za mapema.
Ingawa hoja hiyo haikupita, iliacha athari kubwa katika mchakato wa mageuzi ya sheria za jinsia nchini.
Alihimiza pia kupunguzwa kwa alama za kujiunga na vyuo vikuu kwa wasichana kutoka maeneo kame, kuendeleza uchumi wa wanawake mashinani, na kusaidia wanawake wanaowania viti vya kisiasa.
Katika wasifu wake It is Possible: An African Woman Speaks, Asiyo alisimulia safari yake ya kisiasa akisema ilijaa changamoto, mateso na mafanikio.
Uamuzi wake wa kujiunga na siasa mwaka 1979 uliafikiwa baada ya mashauriano na Baraza la Wazee wa jamii ya Luo na kuungwa mkono na hayati Jaramogi Oginga Odinga.
Alizaliwa katika Kaunti ya Migori na alipata mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Kangaru.
Alianza kazi katika Shule ya Pumwani kabla ya kujiunga na Baraza la Jiji la Nairobi kama mfanyakazi wa kijamii.
Uongozi wake katika MYWO uliwezesha shirika hilo kubadilika kutoka la kufunza kazi za nyumbani hadi kuwa jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi na kisiasa.