Habari za Kitaifa

Tutamsukuma Ruto kutekeleza mkataba wake na Raila, Wanga asema

Na ERIC MATARA, GEORGE ODIWUOR July 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha ODM sasa kinasema kimejizatiti kuhakikisha kuwa mkataba kati ya aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na Rais William Ruto, unatekelezwa kikamilifu.

Akizungumza katika kipindi cha Fixing the Nation katika NTV mwenyekiti wa ODM, Gladys Wanga, alifichua kuwa chama hicho kinakagua kwa makini hatua za utekelezaji wa mkataba huo ili kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu.

“ODM inatathimini utekelezaji wa Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya Ruto na Raila ili kushughulikia masuala yanayohitaji kuimarishwa. Utekelezaji bado haujafikia asilimia 100, lakini tumejizatiti kuhakikisha masuala yaliyoafikiwa yanaendelea kutekelezwa,” alisema Wanga.

“Tulikuwa na kikao hivi karibuni ambapo tulitathmini MoU. Tutakuwa na kikao kingine ili tuangalie hali ya utekelezaji wa MoU.

“Hadi sasa kumekuwa na maendeleo katika masuala kama uundaji wa ajira kwa vijana, lakini kuna mengine ambayo bado hayajatimizwa kama vile fidia kwa waathiriwa wa maandamano ya Gen-Z, ambayo tunaendelea kushinikiza.”

Wakati huo huo, gavana huyo wa Kaunti ya Homabay alisisitiza kuwa ODM itaendelea kutafuta haki kwa mauaji ya kiholela na ukatili wa polisi ikiwa ni pamoja na kisa cha mwalimu Albert Ojwang, hata wakiwa ndani ya serikali.

Bi Wanga alisema kuwa mauaji ya kiholela na ukatili wa serikali si sehemu ya misingi wa ushirikiano huo na ODM itahakikisha inakemea matukio hayo.

“Tunaunga mkono serikali kwa ahadi zake. Usaidizi wetu hauhusu mauaji nje ya sheria au ukandamizaji. Hapa tunaweka mpaka,” alithibitisha.

Wanga alilaani vikali matukio ya hivi karibuni ya ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela kote nchini, na kuomba hatua za kisheria zichukuliwe haraka dhidi ya wahusika.

Mkataba wa Rais Ruto na Bw Odinga, ambao ulizaa Serikali Jumuishi, umekuwa ukikosolewa vikali hivi karibuni kutokana na mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu kwa nguvu.

Katika mahojiano hayo, Bi Wanga pia alisema chama cha ODM kinaunga mkono wito wa Bw Odinga wa mazungumzo ili kutatua masuala mbalimbali yanayozua mgogoro nchini.

Mnamo Machi 7, 2025, Rais Ruto na Bw Odinga walitia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC), ambao walisema utaondoa mvutano wa kisiasa nchini, kuimarisha umoja, na kushughulikia masuala mengine muhimu.

Lakini wachambuzi wa siasa na wataalamu wanasema ahadi nyingi zimeonekana kuwa ngumu kutekeleza kutokana na maandamano yanayoendelea ya vijana wa Kenya kuhusu madai ya mauaji ya kiholela, utawala mbaya na ukosefu wa uwajibikaji.

Bw Odinga ametetea mara nyingi makubaliano yake na Rais William Ruto, akisema yalikusudiwa kupunguza mvutano wa kisiasa, kuimarisha umoja wa kitaifa, na kushughulikia changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi Kenya.