Serikali yaweka breki utekelezaji wa ripoti kuhusu maeneo magumu ya kufanya kazi
SERIKALI imesitisha kwa muda utekelezaji wa mapendekezo mapya ya kufuta baadhi ya maeneo yanayochukuliwa kuwa mazingira magumu kufuatia wimbi la malalamishi kutoka kwa walimu, watumishi wa umma, na viongozi wa kisiasa kote nchini.
Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku alithibitisha kuwa wizara yake kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu imeamua kusimamisha utekelezaji wa ripoti hiyo ili kutoa nafasi ya kutathmini upya maeneo yanayostahili marupurupu ya mazingira magumu.
“Tumeamua kusitisha utekelezaji wa ripoti hiyo kwa sasa. Tunahitaji kuipitia tena kwa pamoja na wadau pamoja na viongozi waliochaguliwa kabla ya kuitekeleza,” alisema Waziri Ruku alipozuru Kaunti ya Samburu.
Walimu na watumishi wa umma kutoka kaunti kama Turkana, Samburu, Marsabit, West Pokot na baadhi ya maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki walielezea hofu kuwa maeneo yao yanaweza kuondolewa kwenye orodha ya maeneo magumu jambo ambalo lingewafanya kupoteza marupurupu yao.
Hata hivyo, Waziri Ruku alihakikishia watumishi wa umma kuwa marupurupu yao hayako hatarini kusitishwa katika tathmini ijayo.
“Wasijali, hakuna atakayepokonywa marupurupu ya mazingira magumu hivi karibuni. Serikali imejizatiti kuhakikisha ushirikishwaji wa umma kabla ya utekelezaji wowote,” aliongeza.
Viongozi wa kisiasa na vyama vya walimu, hususan KUPPET, wameitaka serikali kueleza sababu za hatua hiyo, wakisema inalenga kudhulumu maeneo yaliyotengwa kimaendeleo.
Seneta wa Samburu Steve Lelegwe alisema hatua ya kuondoa Samburu kwenye orodha ya maeneo yenye mazingira magumu na kuiweka kuwa ya ‘kawaida’ ni dharau kwa changamoto sugu zinazowakumba wakazi.
“Huwezi kusema Samburu ni eneo la kawaida ilhali kuna ukosefu wa mtandao, ukame wa muda mrefu, na miundombinu mibovu,” alisema.
Mbunge wa Samburu Magharibi, Naisula Lesuuda pia alilaani hatua hiyo akisema inaleta picha isiyo sahihi ya maisha Samburu na inaongeza pengo la ukosefu wa usawa.
Walimu Samburu, kupitia tawi la KUPPET, pia wamepinga mapendekezo mapya katika Mkataba wa Makubaliano (CBA) wa 2025–2029, wakisema haukuwashirikisha na unawapuuza.
Marupurupu haya hutolewa kwa watumishi wa umma wanaohudumu katika maeneo yenye changamoto kubwa za maisha na kazi. Serikali sasa inakabiliwa na shinikizo la kuhakikisha sera hizo zinatengenezwa kwa usawa na kwa kuzingatia hali halisi ya maeneo husika.