Agizo alilopuuza Uhuru sasa lamtatiza Ruto
KESI inayotaka Rais William Ruto alazimishwe kuvunja Bunge kwa kushindwa kutekeleza kanuni ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili imewasilishwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili ateue jopo la majaji watatu kuisikiliza.
Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Mugambi, kubaini kuwa masuala ya kikatiba yaliyoibuliwa katika kesi hiyo ni sawa na yale yaliyowasilishwa katika kesi tisa nyingine zilizofikishwa mahakamani mwaka wa 2020 na watu binafsi pamoja na taasisi mbalimbali kuhusu suala hilo hilo.
“Baada ya kupitia ombi hili, imebainika kuwa limelenga Spika wa Bunge la Kitaifa, Seneti na Mwanasheria Mkuu kwa kushindwa kutekeleza sheria ya thuluthi mbili baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.
“Pia, uchunguzi wa maombi mengine ulibaini kuwa suala kuu katika kesi hizo ni kushindwa kwa Bunge kutekeleza sheria hiyo licha ya miito ya mara kwa mara inayotolewa kuitekeleza kulingana na Katiba,” alisema Jaji Mugambi.
Kesi hiyo inasisitiza kutekelezwa kwa ushauri uliotolewa na Jaji Mkuu mstaafu David Maraga kwa aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2020, akimtaka avunje Bunge kwa kushindwa kutekeleza sheria hiyo ya usawa wa jinsia.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa mahakamani na wanaharakati Margaret Toili, Eddah Marete na Agnes Ndonji mwaka wa 2022, inalenga Bunge la sasa la 13 kwa msingi kuwa ushauri wa Bw Maraga haukuhusisha tu Bunge la 12 bali Bunge lolote lisilotekeleza agizo hilo la Katiba.
Jaji Mugambi amewasilisha kesi hiyo kwa Jaji Mkuu ili ateue jopo litakaloishughulikia pamoja na nyingine tisa zilizowasilishwa awali kuhusu mada hiyo hiyo.
Alitoa uamuzi huo kutokana na ombi kutoka kwa maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti waliotaka kesi hizo ziunganishwe kwa kuwa zote zilitokana na ushauri wa Bw Maraga uliotolewa Septemba 21 2020.
“Kuna suala la kisheria linalojitokeza katika kesi zote hizi, nalo ni kushindwa kwa Bunge kutekeleza sheria ya thuluthi mbili ya usawa wa jinsia. Suala hili litazidi kujirudia kila baada ya uchaguzi mkuu ikiwa halitatatuliwa kikatiba,” alisema Jaji Mugambi.
Alisema kuwa masuala ya kisheria yaliyo katika kesi zote yanafanana, tofauti ikiwa tu ni wakati ambapo kesi hizo ziliwasilishwa.
Kesi zilizowasilishwa awali zililenga kuvunjwa kwa Bunge lililomaliza muda wake Agosti 2022, huku kesi ya sasa ikilenga kuvunjwa kwa bunge la sasa.
Jaji Mugambi alieleza kuwa suala la kuvunja Bunge kwa kushindwa kutekeleza sheria ya usawa wa jinsia ni suala la kikatiba, la msingi ambalo limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu.
“Kuna haja ya kutolewa kwa tafsiri ya kisheria itakayotoa mwongozo kwa taifa. Haiwezi kusemwa kuwa suala hilo liliisha baada ya bunge la awali kuondoka madarakani,” alisema.
Ni suala la wazi la kikatiba ambalo linahitaji kutatuliwa si tu na bunge la sasa bali pia kwa mabunge yajayo, ili kuepuka kesi za kila mara kuhusu suala hilo hilo la kikatiba.
Wanaharakati hao watatu wanataka wabunge na maseneta wote waondolewe madarakani kwa kushindwa kutekeleza sheria hiyo.
Bi Toili alibainisha kuwa ombi lao linapinga uhalali wa Bunge la 13 kwa kukosa kutekeleza sheria hiyo ya usawa wa kijinsia.
Walipinga kuunganishwa kwa kesi yao na nyingine kwa hoja kuwa jambo hilo litaichelewesha na kuzuia utekelezaji wa sheria hiyo muhimu.
Alisema ombi la kuunganisha kesi hiyo na nyingine halikuwa na msingi wa kisheria na litawasababishia madhara walalamishi.
Hata hivyo, jaji alikubali ombi hilo baada ya kubaini kuwa kesi hizo zina masuala sawa ya kisheria na zote zilitokana na ushauri mmoja wa kikatiba.
Ushauri wa Bw Maraga ulitolewa baada ya Bunge kushindwa kupitisha sheria ya utekelezaji wa sheria ya thuluthi mbili, kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 27(3), kikisomwa pamoja na vifungu vya 81(b) na 100 vya Katiba.
Kukosekana kwa utekelezaji huo kuliibua maagizo manne ya mahakama kuhusu suala hilo.