Kimataifa

Trump ana ugonjwa wa mishipa wa wazee lakini sio hatari, White House yasema

Na  REUTERS, BENSON MATHEKA July 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Ikulu ya White House ilisema Alhamisi kwamba Rais wa Amerika Donald Trump anaugua uvimbe katika miguu ya chini na amepata majeraha madogo mkononi upande wa kulia, baada ya picha kuibuka zikionyesha Trump akiwa na vifundo vya miguu vilivyovimba na vipodozi kufunika sehemu iliyoathirika ya mkono wake.

Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, alisoma barua kutoka kwa daktari wa Trump katika kikao na wanahabari, akisema kuwa matatizo hayo yote mawili ni ya kawaida na si hatari. Alisema uvimbe kwenye miguu unatokana na hali ya mishipa ya damu ambayo ni ya kawaida kwa watu wa umri mkubwa, na mkono wake umeumia kwa sababu ya kushikana mikono mara nyingi.

Kauli hiyo ililenga kukomesha uvumi uliokuwa ukienea mitandaoni kwamba Trump, mwenye umri wa miaka 79, huenda alikuwa anaugua maradhi makubwa kutokana na picha zilizosambaa.

Baada ya kikao hicho, Ikulu ilitoa barua rasmi kutoka kwa daktari wa Rais huyo, Afisa wa Jeshi la Wanamaji  la Amerika, Sean Barbabella, alisema kuwa Trump alifanyiwa vipimo kadhaa kuhusu hali hiyo.

Barua ya daktari huyo ilisema uchunguzi kwa kutumia picha za matibabu ulionyesha kuwa Rais ana “ ugonjwa wa mishipa”, hali isiyo hatari na ya kawaida kwa watu walio na umri zaidi ya miaka 70.

Daktari huyo alibainisha kuwa hakuna dalili yoyote kuwa Trump ana maradhi ya mishipa ya damu mikuu. Vipimo vya ziada pia havikuonyesha matatizo ya moyo, figo, au ugonjwa wa mwili kwa ujumla.

Leavitt aliongeza kuwa Rais Trump hapati maumivu yoyote kutokana na hali hiyo ya mishipa.

Katika picha za Julai 15, mkono wa kulia wa Rais Trump ulionekana umefunikwa na vipodozi. Daktari Barbabella alisema aliona majeraha madogo kwenye ngozi ya nyuma ya mkono wa kulia, ambayo yanaendana na maumivu ya tishu laini kutokana na kushikana mikono mara kwa mara, pamoja na matumizi ya aspirini ambayo Trump hutumia kama sehemu ya mpango wa kiafya wa kuzuia magonjwa ya moyo.

“Rais Trump bado yuko katika hali bora kiafya,” alisema Barbabella.

Daktari Kwame Amankwah, mkuu wa upasuaji wa mishipa katika Chuo Kikuu cha Connecticut, alisema hali hiyo ya mishipa ni ya kawaida kwa watu wazee na hutokea pale mishipa  mikuu ya damu inashindwa kupeleka damu kwa moyo vizuri.

Amankwah alisema hali hiyo hutibiwa kwa kuvaa soksi za shinikizo na kuinua miguu juu. Aliongeza: “Hata kama hana ugonjwa wa moyo, hali hii inahitaji kushughulikiwa. Isipopatiwa matibabu, uvimbe mkubwa na vidonda vinaweza kuanza kujitokeza.”

Daktari mwingine, Todd Berland wa NYU Langone Health, alisema hali hiyo haiathiri muda wa maisha ya mtu, bali hubadilisha hali ya maisha kwa ujumla.

Trump alifanyiwa uchunguzi wa kina wa kimwili mnamo Aprili 11 katika Kituo cha Matibabu cha Jeshi la Walter Reed, ambapo ilibainika kuwa moyo wake una mpigo wa kawaida na hakuwa na matatizo yoyote makubwa ya kiafya.