Kuporomoka kwa viwanda vya sukari kulivyoua miji, uchumi
Nabii Yohana, anayejiita nabii na kudai kuwa na nguvu kutoka kwa Mungu, huenda sasa anapaswa kuombea kijiji chake cha Nandolia katika Wadi ya Bukembe Magharibi, Kanduyi, Kaunti ya Bungoma.
Nandolia, kijiji kilichokuwa na shughuli nyingi miaka ya 1970 wakati kampuni ya Nzoia Sugar ilipoanzishwa, sasa kimetulia na kimekuwa kimya na kujawa na kutu.
Kutu hiyo ya rangi ya kahawia imeenea katika paa za maduka kandokando ya barabara, mashine zilizotelekezwa, matrekta, na trela kwenye kiwanda cha Nzoia Sugar.
Kiwanda cha Nzoia Sugar ambacho kilianzishwa miaka ya 1970 kilileta uhai kijijini humo na kusababisha shughuli nyingi za kiuchumi.
‘Ni Nzoia Sugar iliyowezesha watu wa huku kujenga nyumba za mabati na kusomesha watoto wao,’ asema Saulo Busolo, aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Sukari ya Kenya ambaye sasa ni mkulima.
Leo hii, baada ya kiwanda hicho cha serikali kuporomoka, kijiji kimekuwa kimya.
Albert Kimoli, mshonaji viatu, ametumia miaka 15 iliyopita kushonea viatu wafanyakazi wa Nzoia Sugar. Lakini baada ya kampuni hiyo kufuta kazi asilimia 70 ya wafanyakazi wake kutokana na matatizo ya kifedha, biashara imeyumba sana.
‘Hapo zamani, wateja walikuwa wakirudi haraka kuchukua viatu vyao,’ asema. ‘Siku hizi, wateja hawarudi kabisa.’
Hali ni sawa katika vijiji vilivyo karibu na viwanda vya sukari vya serikali vilivyo katika hali mbaya, na kusababisha miji kuporomoka katika ukanda unaokuzwa miwa.
Hali hii inaonekana katika mji wa Mayoni karibu na kiwanda cha Mumias Sugar, Muhoroni na Chemelil katika Kaunti ya Kisumu, na pia Sony katika Kaunti ya Migori.
Unapofikiria kuhusu sekta ya sukari, labda unawaza mashamba ya miwa. Lakini athari zake zinasambaa katika uchumi mzima wa eneo hilo.
Kiwanda kimoja cha sukari hakisagi miwa tu. Kinaajiri maelfu ya watu — kutoka kwa wafanyakazi wa kiwandani hadi maafisa wa mashambani. Halafu kuna wakulima, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo, wanaotegemea malipo ya miwa kulisha familia zao, kulipa karo na kuendeleza biashara ndogo ndogo.
Dereva wa lori anayesafirisha miwa, wachuuzi wa vyakula kandokando ya barabara, maseremala na wauzaji wa pembejeo — wote hutegemea sekta hii. Wakati kiwanda kinafanya kazi, pesa huzunguka. Vijiji vina uhai. Miji midogo hustawi.
Sasa fikiria kile kinachotokea wakati mfumo huu unapovunjika — kiwanda kikifungwa kwa sababu ya usimamizi mbaya au uhaba wa miwa. Athari zake haziishii kwa wafanyakazi wa kiwanda. Jamii nzima huathirika.
Chukulia mfano wa Mayoni, karibu na Mumias Sugar katika Kaunti ya Kakamega — mji mwingine uliofifia katika ukanda wa miwa.
‘Mayoni, mji ule ulioupita ukija, zamani ulikuwa kama London ya eneo hili,’ asema Saulo Busolo.
Tulipowasili Mayoni siku ya Jumatatu alasiri, nusu ya maduka yalikuwa yamefungwa.
Mbali na shamba kubwa la miwa, moshi ulionekana ukifuka kutoka Mumias Sugar. Lakini moshi huo haukuleta matumaini wala kupunguza hasira za vijana wa eneo hilo, wengi wao wakidai mwekezaji mpya, Sarrai Group, hajawasaidia wenyeji kupata ajira.
Mayoni Bar & Restaurant, anakumbuka Ramadhan Wataka Otembo mwenye umri wa miaka 65, lilikuwa jengo la kwanza la ghorofa katika Mumias nzima.
Zamani, baa hiyo ilikuwa maarufu sana, na iliwavutia wageni kutoka maeneo mbalimbali, kwa mujibu wa Otembo.
‘Lakini siku hizi ukienda huko, utakuta watu wanakunywa uji na mandazi tu,’ asema.
Wakati wa utawala wa Booker Tate — kampuni ya kimataifa iliyosimamia Mumias Sugar — kampuni hiyo ilitenga ekari nne kutoka shamba lake la ekari 8,700 kujenga vibanda vya jua kali kwa wenyeji.
‘Vyote hivyo sasa vimesahuliwa watu wanaishi ndani badala ya kuvitumia kufanyia kazi,’ asema Moses Malala, mwenyekiti wa Soko la Mayoni.