Profesa Ng’eno alitetea utoaji maziwa ya Nyayo
Profesa Jonathan Kimetet arap Ng’eno alipitia vipindi tofauti kabisa hadi mwisho wa maisha yake.
Alikuwa waziri katika serikali ya Rais Daniel arap Moi, akaelea kwenye wimbi la siasa, akashuka, akaruka tena na kushuka tena, hatimaye alifariki akiwa na umri wa miaka 61, Moi bado akiwa madarakani.Ng’eno (pichani) alijiunga na siasa mwaka 1979 na kupanda ngazi serikalini kwa kasi isiyotarajiwa.
Hadi mwaka huo, hakujulikana sana katika jamii ya Kipsigis katika Kaunti ya Kericho, wala katika siasa kwa ujumla.Profesa huyo, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi Nakuru Millers, kampuni ambayo haikuwa ikijulikana na wengi iliyosemekana kuwa na uhusiano na Moi, alijitosa katika siasa katika uchaguzi uliofanyika baada ya kifo cha Rais Jomo Kenyatta Agosti 22 ,1978.
Moi, ambaye alikuwa Makamu wa Rais kwa miaka 12, aliingia mamlakani mwaka uliofuata.Dkt Taita arap Towett, aliyekuwa Waziri wa Elimu chini ya Kenyatta, alikuwa kiongozi muhimu katika eneo la Kipsigis.
Towett, alikuwa Mbunge wa Buret na pia rafiki wa rika na Moi, na alikuwa miongoni mwa wahusika wakuu katika harakati za kupigania uhuru Kenya.Moi alikusudia kubadilisha siasa nchini moja kwa moja baada ya kifo cha Kenyatta kwa kuleta wanasiasa wapya waliokuwa waminifu kwake. Kabla ya 1979, alifanya mkutano Kapkatet, na kumwambia Towett aondoke kwenye siasa.
Towett, aliondoka moja kwa moja na kufuta miaka 30 ya maisha yake ya siasa ambayo alipata mafanikio makubwa.Baada ya hapo, Ng’eno, akiwa na umri wa miaka 43, alianza kutembea eneobunge la Buret akiwa na Ayub Chepkwony, msaidizi wa Moi alipokuwa makamu rais.
Ng’eno alishinda tiketi ya KANU na kiti cha ubunge cha Buret, na baadaye Moi alimpa wadhifa wa Waziri wa Maendeleo ya Maji.Ng’eno aliteuliwa Waziri wa Elimu ya Msingi, Moses Mudavadi, alipokashifiwa kwa kuajiri walimu wengi wa jamii yake ya Waluhya.
Uchunguzi wa umma ulisababisha Moi kufanya mabadiliko ya baraza la mawazari ambapo Ng’eno alihamishiwa Wizara ya Elimu ya Msingi na Mudavadi akatua Wizara ya Maji.
Ng’eno alihudumu katika wizara hiyo hadi uchaguzi mkuu wa 1983.Baada ya uchaguzi, Moi aliunganisha Wizara ya Elimu ya Msingi na Sayansi na Teknolojia na kumteua Ng’eno kuisimamia wizara iliyopanuliwa.
Lakini alikumbana na changamoto nyingi kati ya 1983 na 1985, hasa mpango wa maziwa ya bure katika shule za msingi ulioanzishwa Machi 15, 1979 kwa gharama ya Sh170 milioni kwa wanafunzi 3.2 milioni; idadi hiyo iliongezeka mara mbili.
Programu hiyo ilikabiliwa na siasa, rushwa, matatizo ya ugavi na usambazaji.Programu ya maziwa ilianza kama majaribio katika wilaya nane kabla ya kusambazwa kitaifa.
Ilisemekana kwamba maziwa yalichanganywa na kemikali. Watoto waliripoti maumivu ya tumbo, lakini uchunguzi wa wataalamu uliondoa tuhuma hizo.
Changamoto ya pili ilikuwa usafirishaji, uhifadhi na usambazaji kitaifa. Wadau walifanya biashara hiyo kama chanzo cha pesa. Walimu pia walishirikiana kuchukua maziwa na kuuza au kutumia nyumbani. Rushwa ilikuwa changamoto kubwa ya tatu; fedha zilizotolewa hazikutumika vyema.
Ng’eno alikabiliwa na maswali mengi bungeni na nje kuhusu mpango huo. Hatimaye, mpango huo ulififia baada yake kuondoka wizarani.Zaidi ya hayo, Ng’eno alipambana na migomo ya wanafunzi na walimu katika vyuo vikuu.
HELB ilikuwa na shida kubwa katika kurejesha mikopo; sheria iliundwa bungeni baada yake kuondoka ambayo iliruhusu mikopo kukatwa moja kwa moja na mwajiri. Idadi ya wanafunzi iliongezeka bila fedha za kutosha kuwasaidia wote.Alihamishiwa Wizara ya Makazi kabla ya uchaguzi wa mlolongo wa 1988, ambapo alihudumu kwa muda mfupi.
Lakini kazi yake ya kisiasa iliporomoka mwaka wa 1988 wakati aliyekuwa Hakimu Timothy Mibei alipomshinda katika uchaguzi wa kiti cha eneobunge la Buret.Kwa miaka mitano alikaa nje ya siasa.
Lakini alirejea 1991 baada ya kujiuzulu kwa Spika wa Bunge Moses arap Keino. Mei 12, 1991, Keino aliwasili Bungeni na bila arifa yoyote, aliandika barua ya kujiuzulu, akaionyesha na kuondoka. Moi alipata habari na akamuita Ng’eno Ikulu Juni 11 1991.
Ng’eno alichaguliwa kuwa Spika wa nne wa bunge la Taifa, na kurejea rasmi katika siasa kabla ya uchaguzi wa 1992.Alihudumu tu kwa miezi 18 kabla ya kurudi kujihusisha na siasa, na Moi akampokea tena na kumteua waziri wa Kazi ya Umma na Makazi.
Ng’eno alishindwa tena katika uchaguzi wa 1997 na mwalimu Paul Sang, mara hii kwa mara ya mwisho.Alizaliwa mwaka 1937 huko Buret, akasomea shule za hapo kabla kwenda Amerika alipopata shahada katika Uchumi, Siasa na Falsafa.
Alifundisha vyuo vikuu nchini Amerika kabla ya kurudi Kenya. Kabla ya kufariki kwake Juni 11 1998, siasa za jamii ya Kipsigis zilikuwa zimebadilika tena, zikihusisha Kipkalia Kones na John Koech ambao pia walihudumu kama mawaziri chini ya utawala wa Moi.